Julio: Simba ina wachezaji 12 tu

SIMBA imebeba ubingwa kwa rekodi ikiwa imesaliwa na mechi sita mkononi lakini kocha mwenye mapenzi makubwa ya klabu hiyo, Jamhuri Kihwelu Julio amedai timu hiyo ina wachezaji 12 tu wenye hadhi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.

Julio alisema Simba ilistahili kunyakua ubingwa kutokana na wachezaji waliokuwa nao na viwango walivyokuwa wakivionyesha na kuweza kushindana na timu nyingi na kuvishinda.

“Ubingwa wa Simba unatakiwa na vilabu vingine kutafuta wachezaji wenye kuleta ushindani na kupata wafadhili ili kuacha kuwa tegemezi na fedha zinazotoka TFF ndio maana timu nyingi wachezaji wanacheza kwa unyonge kwa maana wanakuwa hawalipwi kwa wakati.

“Timu inapokuwa na uchumi mzuri inasaidia pia kupata ushindani ndiyo maana walipoteza kwa Mwadui FC sio kwamba kwa kubahatishwa bali kule nako kuna wachezaji wazuri japo wanakosa morali,” alisema Julio ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba.

“Simba ina wachezaji wazuri hata ukiangalia Chama (Clatous), Kahata (Francis) na Mkude (Jonas) na wengine kama tisa au kumi ambao wanaweza kwenda nao kwenye mashindano ya kimataifa waliosalia wazuri kwa ligi ya nyumbani.

“Angalia tunapotoka nje tunapoteza kwa idadi kubwa ya mabao halafu nyumbani ndio tunaambulia bao moja, hiyo inaonyesha bado hatujajipanga, hivyo Simba wanatakiwa kufanya usajili wa kukomaa na sio wa kuangalia watu kwa sababu unamjua.”

Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Mohamed Rishard ‘Adolf’ alisema; “Nina uhakika itawakilisha vyema nchi kwenye mashindano ya kimataifa japo siwezi kusema kitu gani wanatakiwa kukifanya maana sio nafasi yangu ya kufanya hilo.

“Imekuwa ikifanya vizuri kuanzia kwenye ligi na hata inapopata nafasi lakini naamini wakijiandaa watafanya vizuri msimu huu,” alisema Adolf.