Imekwisha hiyo, Jardon Sancho anatua Man United

MANCHESTER United imeandaa ofa ya Pauni 50 milioni ili kuhakikisha wanaipata saini ya winga wa Borussia Dortmund, Jadon Sancho, ambaye ana thamani ya Pauni 100 milioni kwenye mkataba wake wa sasa unaotarajiwa kufikia tamati mwaka 2022.

Suala hilo limeifanya Dortmund kuanza kutafuta mbadala wa mchezaji huyo kwa kuwa wanaamini United inaweza kufanikiwa kutoa kiasi cha fedha wanachohitaji. Inaelezwa kuwa Dortmund huenda ikawa tayari kupokea Pauni 50 milioni ikihofia kumpoteza bure wakati msimu ujao utakapofikia tamati.

United imekuwa ikiifuatilia saini ya mchezaji huyo kwa muda mrefu ambapo wamekuwa wakipambana na Real Madrid wanaotajwa kuwa kwenye mpango wa kuhakikisha wanaipata saini ya fundi huyo. Sancho (20), amekwishaweka wazi kuwa anatamani kujiunga na United dirisha lijalo ikiwa makubaliano kati ya pande hizo yatafikiwa.