IMETOSHA Zilikuwa Siku 75 ngumu kwelikweli

KAMA hujui ni kwamba zimeshapita jumla ya siku 75 tangu shughuli zenye mikusanyiko ya watu, ikiwamo michezo ilipositishwa na serikali Machi 17 kutokana na janga la virusi vya corona.

Serikali kupitia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ilitoa tamko hilo kutokana na kugundulika kuingia kwa virusi hivyo vinavyosababisha ugonjwa wa covid-19 unaosambaa kwa kasi na kuteketeza uhai wa wanadamu tangu ulipobainika Novemba mwaka jana katika mji wa Wuhan, China.

Kutokana na marufuku hiyo, michezo na burudani zilikoma na kuwaacha mashabiki kwenye ukiwa, hasa wanaofuatilia Ligi Kuu iliyokwamia raundi ya 29, lakini ndani ya siku hizo 75 za kusimama kwa ligi kuna matukio kadhaa ya huzuni na kusisimua yametokea na Mwanaspoti imeyadadavua.

KAMBI STARS YAVUNJWA

Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) lilitangaza kuvunja kambi ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ iliyokuwa imewekwa kujiandaa na michuano ya Chan 2020.

Uamuzi huo ulikuja katika kutekeleza agizo la serikali ya Tanzania kuhusu kujikinga na virusi vya corona.

Michuano ya Chan ilipangwa kuchezwa kati ya Aprili 4-25 nchini Cameroon na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), lilitangaza kufuta kabisa mashindano hayo kwa muda ambao ulipangwa kutokana na janga hilo ambalo liliikabili dunia nzima.

Caf haikuahirisha Chan 2020 tu, bali lilisimamisha mechi zote za kufuzu za mashindano ya Afrika kwa ushauri wa Shirika la Afya Dunani (WHO), kutokana na mlipuko wa virusi covid 19 hadi hapo itakapoamuliwa vinginevyo.

Mechi zilizofutwa ni za tatu za na za nne kufuzu fainali za Kombe za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2021, ambazo zilipangwa kufanyika kati ya Machi 25 na 31 mwaka huu.

Nyingine ni za kufuzu fainali za Kombe la Dunia la Wanawake chini ya umri wa miaka 20, zilizopangwa kufanyika kati ya Machi 20 na 22, na marudiano Machi 27 na 29 mwaka huu.

Aidha, Caf pia ilisitisha mechi za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa (Afcon) kwa Wanawake 2020 zilizopangwa kufanyika kati ya Aprili 8 na 14 mwaka huu.

VIFO

Wakati taifa na dunia kwa ujumla wakipitia katika wakati mgumu la zuio la michezo, hapa nchini kumetokea misiba ya watu mbalimbali kutoka katika nyanja ya soka, siasa, muziki na nyinginezo ambazo tukianza kuwaandika wote hawa tunaweza kumaliza ukurasa mzima.

Miongoni mwa vifo ambavyo vimetokea hapa nchini, Mei 25, beki wa zamani wa klabu ya Yanga, Lawrance Mwalusako alifariki dunia alfajiri katika hospitali ya taifa Muhimbili alipokuwa amelazwa kwa matibabu kwa kilichoelezwa kusumbuliwa na kiharusi.

Siku moja kabla ya Mwalusako aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Yanga, sekta ya muziki ilipata pigo kwa kuondokewa na mwanamuziki mkongwe wa Kilimanjaro Band ‘Wana-Njenje’, Mabrouk Hamis Omar ‘Babu Njenje’.

Lakini kabla ya hapo mdau mkubwa wa michezo na mwanachama maarufu wa Simba aliyekuwa Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa naye aliaga dunia ndani ya Aprili sambamba na wanasiasa wengine akiwamo Mchungaji wa Kanisa la Mlima wa Moto, Askofu Gertrude Rwakatare, aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Augustine Mahiga, Jaji Mkuu mstaafu, Augustine Ramadhani na vifo vingine kadhaa kikiwamo cha baba wa nahodha wa timu ya taifa ya wanawake, Asha Rashid ‘Mwalala’, Mzee Rashid.

FIFA YABADILISHA KANUNI

Katika kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa, Shirikisho la Soka Dunia (Fifa) lilitangaza kanuni mpya ya kuzuia wachezaji kutema mate uwanjani ambapo anayefanya hivyo ataonywa kwa kadi ya njano na kama akizingua zaidi atalimwa nyekundu moja kwa moja. Huku pia ikizuia klabu na wachezaji waliokuwa mikataba yao ipo mwishoni kuendelea kuhesabika ndani ya timu zao mpakia misimu ya ligi ya kila nchi husika itakapokamilishwa.

UBINGWA WA MEZANI

Uholanzi waliamua kuufuta msimu wao mzima, lakini Ubelgiji, Ufaransa, DR Congo na baadhi ya nchi ziliamua kuzipa klabu zao ubingwa wa mezani kutokana na janga la corona na nafasi walizokuwa nazo timu hizo.

PSG, TP Mazembe, Club Brugge wameshatawazwa mabingwa, huku Gor Mahia waliotangazwa awali na FKF wakigomewa na KPL, ingawa kwenye nchi nyingine zimeamua kukomaa na sasa Bundesliga inaendelea, huku EPL, La Liga na hata VPL ya Tanzania Bara na ligi ya Zanzibar zikiwa njiani kuanza ndani ya mwezi huu wa Juni.

MABOSI KITANZINI

Likaibuka suala jingine la matumizi mabaya ya zaidi ya Sh. 1 bilioni, pesa za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ambazo alitoa kwa ajili ya kuwa wenyeji wa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) U-17 zilizofanyika hapa nchini mwaka jana katika viwanja viwili Taifa na Azam Complex.

Mabosi wengi wakubwa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), waliitwa katika ofisi ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), ili kuhojiwa kuhusiana na suala hilo ambalo liligusa idara mbalimbali hapa nchini.

Mei 19, Katibu Mkuu wa (TFF), Wilfred Kidao alitia timu katika ofisi za TAKUKURU, kwa ajili ya kufanyiwa mahojiano kuhusu suala hilo ambalo hadi sasa bado liko katika hatua ya uchunguzi kwani bado majibu hayajatolewa kama watu wengi ambavyo wanatamani kujua.

BAO LA SAMATTA

Bao alilofunga Mbwana Ally Samatta akiwa KRC Genk ya Ubelgji dhidi ya Liverpool kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Novemba 5, 2019 kwenye Uwanja wa Anfield liliteuliwa kuwa bao bora la msimu na klabu yake hiyo ya zamani iliyochapwa 2-1 siku hiyo.

Ni Januari tu mwaka huu KRC Genk ilimuuza Mbwana Samatta kwa klabu ya Aston Villa baada ya kuwa naye tangu Januari 2016 ilipomnunua kutoka TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Samatta aliyekuwa anacheza Anfield kwa mara ya kwanza Novemba 5 mwaka jana, aliifungia KRC Genk bao hilo katika dakika ya 40, kwa kichwa akimalizia krosi ya kiungo Mbelgiji, Bryan Heynen.

RAGE MATATANI TAKUKURU

Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba, Ismael Aden Rage alishikiliwa na taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa tuhuma za rushwa na kuanza kampeni za uchaguzi mkuu kabla ya wakati.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tabora, Mussa Chaulo ilisema kuwa Mei 23, mwaka huu Rage ambaye ni Mkurugenzi wa Voice of Tabora alishikiliwa baada ya TAKUKURU kupata taarifa kutoka chanzo cha siri kikieleza kuwa Mbunge huyo wa zamani wa Tabora Mjini amedaiwa kuanza kampeni za uchaguzi kabla ya wakati.

Taarifa hiyo ya siri iliyotolewa ilieleza kuwa kiongozi huyo wa zamani wa Simba akiwa katika maeneo kadhaa ndani ya Manispaa ya Tabora kwa nyakati tofauti alikusanya wapiga kura ambao ni viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya kata na matawi kwa lengo la kuwashawishi ili wampigie kura.

WASIKIE WADAU

Siku chache baada ya serikali kutangaza kurejesha michezo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Almasi Kasongo alitangaza Ligi itaanza Juni 13 na ratiba ilitarajiwa kutoka jana na kumwagia sifa Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa kuwaruhusu kuendelea na michezo.

“Tulikutana na hali ngumu kipindi ligi imesimama kwani jukumu letu kubwa kuona tunakuwa na ligi nzuri ambayo inakuwa kila siku kwa maana hiyo kukosekana kwake ndio ilikuwa shida zaidi kwa upande wetu,” anasema Kasongo.

Kwa upande wa winga wa Kagera Sugar, Godfrey Mwashuiya anasema wakati ligi akiwa imesimama walikuwa kama hawatendi haki kwani kwa upande wao wachezaji wa Kagera walikuwa wanalipwa kila kitu kwa wakati kama ligi bado inaendelea.

“Kwa maana hiyo kuchukua pesa kutoka kwa mabosi zetu bila kufanya kazi ni kama tulikuwa tunawadhulumu kwa maana hiyo kurudi kwake limekuwa jambo la furaha kwetu kufanya kazi ambayo tunaitolea jasho na tunastahili kulipwa.