Huyu Yondani, yaani basi tu

YANGA imejiweka kwenye wakati mgumu baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Pyramids ya Misri katika mechi ya mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika uliopigwa jana katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Licha ya Yanga kujituma vilivyo, ujanja na mbinu za wapinzani wao ziliwaangusha, huku beki Kelvin Yondani akionyesha umahiri mkubwa katika majukumu yake kabla ya kutolewa nje kwa kadi ya pili ya njano iliyoambatana na nyekundu wakati akiinusuru timu yake.

Hapa chini ni namna nyota wa Yanga walivyocheza kwenye mchezo huo na alama walizopata chini ya kumi.

Farouk Shikhalo - 7

Alicheza dakika 90 za mchezo akilinda lango. Katika kipindi cha kwanza pekee aliokoa mashuti manne kiufundiambayo yangeweza kuzalisha mabao. Alifanya hivyo pia katika katika kipindi cha pili. Licha ya kuruhusu mabao mawili, hakuna lawama zilizoenda kwake.

Juma Abdul - 6

Alicheza katika nafasi yake ya beki wa kulia. Alionekana kutanguliza majukumu ya ulinzi kuliko kushambulia kutokana na kubanwa vizuri. Hakuweza kuzalisha krosi zake zilizozoeleka kama kawaida yake.

Ally Sonso - 3

Alionekana imara katika upande wa beki ya kushoto ndani ya dakika mbili za kipindi cha kwanza shuti lake kali moja lilikiwa shambulio zuri. Changamoto pekee upande wake ulipitisha mabao yote mawili ya Pyramids akiwa amepanda mbele kusaidia mashambulizi. Pia alimsababishia kadi nyekundu Kelvin Yondani kwa pasi yake fupi dakika za mwisho.

Ali Ali - 5

Beki wa kati aliyecheza sambamba na Kelvin Yondani, alipambana kutuliza safu ya ulinzi lakini bado ugeni katika eneo hilo ulimpa shida akionekana kupishana zaidi kimawasiliano na wenzake na kipindi cha kwanza almanusura ajifunge kwa kichwa kama kawaida yake lakini mpira ukatoka.

Kelvin Yondani - 7

Uzoefu wa kucheza kwake mechi nyingi ndani ya kikosi hicho bado unambeba mkongwe huyu. Kipindi cha kwanza tu alifanya kazi ya ziada akiokoa shambulizi kali la Pyramids akiwa katika mstari wa bao wakati kipa akiwa ametoka kucheza krosi. Alionekana kutulia akiwazuia vyema nyota wa wapinzani wao. Bahati mbaya sana akapewa kadi nyekundu akiisitiri timu yake isizame zaidi kwa kufungwa bao la tatu baada ya Sonso kupiga pasi fupi.

Abdulaziz Makame -6

Alicheza nafasi ya kiungo wa ulinzi katika kikosi cha Yanga. Kuna wakati alikuwa anaonekana kutulia zaidi na kusambaza mipira lakini mingi hata hivyo haikuwa na madhara kwa wapinzani. Alionyesha ushindani mkubwa katika eneo la kiungo na kuwafanya Pyramids kushambulia kutokea pembeni

Feisal Salum - 7

Licha ya kutolewa kipindi cha pili kumpisha Juma Balinya, kiungo huyu alicheza vizuri. Alikaba na kujaribu kusogeza mashambulizi mbele na pia alijaribu mara mbili kufunga kwa mashuti yake makali, lakini kizuizi kikawa kipa wa Pyramids na timu ya taifa ya Misri, Ahmed El Shenawy.

Mapinduzi Balama -6

Alionekana kuhangaika kupandisha mashambulizi lakini hakuwa na mbinu zaidi za kupenya kama kawaida yake ingawa kasi yake ilikuwa tishio kubwa kwa Pyramids na kumpa ulinzi mkali asilete madhara.

Mrisho Ngassa 3

Hakuwa na madhara yoyote katika mchezo, kitu kibaya zaidi makosa yake akifanya madoido ya kumdanganya kiungo wa Mohamed Farouk kuwa akitaka mpira utoke, kisha ukanaswa na kuzalisha bao la pili lililoikandamiza zaidi timu yake. Pengine bila kosa hilo Yanga ingepata sare.

Papy Tshishimbi - 5

Nahodha wa timu, hakuwa vizuri sana. Bahati ni kwamba aliifungia timu yake bao pekee lililopunguza makali ya kipigo hicho baada ya kumfinya beki hadi akakaa chini kabla ya kupiga la shuti la ufundi lililojaa wavuni. Jana hakuwa na mchango mkubwa katika kucheza sambamba na mshambuliaji wa mwisho Sadney Urikhob.

Sadney Urikhob - 5

Hakuwa katika ubora wake, inawezekana labda ni kutokana na kutokuwa fiti kwa asilimia 100 kiafya. Jambo kubwa aliwatisha mabeki wa Pyramids japo hakuwa na shambulizi lolote kali na hakuwa na uimara wa kuwapita mabeki wa wapinzani wao.

Deuse Kaseke - 4

Aliingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Makame. Alipata nafasi moja pekee atakayoikumbuka baada ya kuunasa mpira uliopanguliwa na Shenawy kutokana na shuti la mpira wa friikiki ya Balinya. Kama angetulia angeweza kutoa pasi kwa Yondani ama Ally Ally waliokuwa katika nafasi nzuri ya kufunga kuliko shuti lake lililopaa juu.

Balinya - 4

Mpira wake wa friikiki ulipanguliwa na kipa Shenawy na kumnyima bao. Aliingia sub.