Hili nalo ni ajabu jingine la Ligi Kuu

TULIA buana. Si mnakumbuka tuliwahi kuandika maajabu kadhaa ya Ligi Kuu Bara? Sasa unaambiwa yale maajabu katika soka la Bongo, wala hajayaisha kwani tukio lililoibuka juzi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kwenye mechi ya Simba dhidi ya Coastal Union, limefichua madudu mengine.

Ni hivi. Watetezi wa ligi hiyo, Simba jioni ya leo Ijumaa watakuwa Uwanja wa Uhuru kuikaribisha Kagera Sugar wakiwa na kiu ya kulipa kisasi cha 2-1 walichopewa mjini Bukoba, wakitoka kupata ushindi wa kishindo wa mabao 8-1 dhidi ya Coastal Union.

Katika pambano lao la juzi dhidi ya Wagosi, nyota wake wawili, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi walifunga ‘hat trick’ na kukabidhiwa mipira, lakini usichojua ni kwamba mipira ile haikutumika kwenye mchezo huo kabisa, bali walichomolewa stoo na wakakabidhiwa zawadi zao.

Inawezekana hujaelewa. Kwa kawaida anayefunga ‘hat trick’ anapewa tuzo ya mipira iliyotumika kwenye mchezo husika, lakini mipira waliyopewa Okwi na Kagere kama tuzo ya kila mmoja ya kufunga ‘hat trick’, ilichomolewa sehemu kwa vile iliyotumika ilikuwa ni ya Simba na wala siyo ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wala Bodi ya Ligi (TPLB).

SIRI NZITO

Inaelezwa kuwa, kwa msimu huu wote, Simba imekuwa ikitumia mipira yao katika kila mchezo wanaocheza katika Ligi hiyo, huku wasimamizi wa ligi wakikosa kabisa mipira ya kuitumia uwanjani kitu ambacho ni maajabu mengine ya soka la Tanzania. Acha kushangaa kabisa.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alifichua kuwa, msimu huu katika mechi zao zote wamekuwa wakitoa mipira yao katika kila mchezo ambao watacheza kwani ile iliyoandaliwa na TFF, waliyogaiwa kila timu ili kutumia katika mechi si mizuri na haina viwango.

Rweyemamu alisema mipira ambayo tulipewa na TFF, ni kama ile ambayo walipewa zawadi Kagere na Okwi walipofunga mabao matatu kwenye mechi ya Coastal Union, lakini si bora kwa kuchezea kwani ni myepesi na inapepea kwa upepo na hata kwa mazoezi haifai.

“Ukiondoka mechi kubwa ambazo tumecheza, michezo mingine yote ya mikoani na hapa Dar es Salaam, tumekuwa tukitoa mipira yetu 10 ili kuitumia katika kila mchezo husika kwani yetu ipo katika hali nzuri ya kuchezea na mara baada ya kumaliza tunaichukua.

“Katika mechi ya Coastal baada ya kumalizika tulichukua mipira yetu yote kama kawaida Kagere na Okwi walipewa zawadi ile mipira ya kawaida ambayo haikutumika ambayo si ya kwetu,” alisema Rweyemamu.

SIKIA HII SASA

Mtoa taarifa aliidokeza Mwanaspoti kuwa, mbali ya Simba kutumia mipira yao katika mechi zao, lakini mechi za mikoani kama walizocheza dhidi ya Biashara United walipoteza mmoja na kurudi tisa na kwenye mchezo wa Kagera Sugar ambao walipoteza kwa kufungwa mabao 2-1, kuna ambayo ilifichwa ili kutumika ile ambayo si bora katika kuchezea.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mnguto, alithibitisha kuwapo kwa uhaba wa mipira.

“Ni kweli msimu huu kuna tatizo la uhaba wa mipira kwenye mechi za Ligi Kuu Bara na si Simba ambao, wanatumia mipira yao, bali hata timu nyingine wanapokuwa wanacheza wanatumia mipira yao.”

Mnguto alisema Simba wameonekana kutumia mipira yao ni kutokana wamekuwa wakifuatiliwa katika mechi zao, ila si pekee wanaotumia bali ni timu zote huwa zinafanya hivyo, kwani Ligi haina mdhamini.

Alisema mipira ya kutoa zawadi kama mchezaji akifunga mabao matatu katika mchezo mmoja (hat trick), ipo lakini ile ya kuchezea katika hali ya ushindani ndiyo tatizo kwetu msimu huu baada ya kukosa mdhamini, ila msimu ujao litaisha hili na halitakuwapo tena kwani tutajipanga kuwa na mipira ya kutosha na yenye viwango vya kimataifa.

“Juhudi kubwa za kumtafuta mdhamini kwa upande wetu zinafanyika, lakini miongoni mwa makubaliano ambayo tutaingia naye ni kutupatia mipira iliyokuwa bora na tutaigawa katika kila kituo ili kuweza kutumika katika mechi za ligi na kuondoa kabisa uhaba ambao, tumekutana nao msimu huu,” alisema Mnguto.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Salum Chama alisema katika kituo cha Kanda ya Ziwa pale Bukoba ana mipira miwili tu ambayo inatumika katika mechi za Ligi Kuu Bara na kabla ya mchezo wowote kuchezwa, huwaeleza viongozi wa timu husika kufika na mipira yao.

Alisema maelekezo hayo hutolewa wakati wa kikao cha maandalizi ambacho kwa kawaida hufanyika asubuhi kabla ya mchezo husika jioni.

“Siku ya mechi huwa nakwenda katika kikao na mipira miwili na baada ya hapo nawaambia viongozi wa timu waje na mipira yao mitatu ili kuweza kusaidia na kutumika katika mchezo ambao utachezwa jioni,” alisema na kuongeza;

“Kama ikitokea kuna mchezaji amefunga hat trick kwa pale huwa tunaonyesha kama tumemkabidhi na kumpiga picha, lakini baada ya hapo lazima tuichukue kwani akiondoka nao tutabaki bila mpira.

“Kama mchezaji atahitaji kuupata mpira wake itabidi anapokuwa Dar es Salaam aende ofisi za TFF kwa ajili ya kupewa mpira wake ama anaweza kusubiri hadi nitakapokwenda huko ndio nitarudi na mpira wake,” alisema Chama.