HISIA ZANGU: ‘Happy Birthday’ nyingine chungu kwa Erasto Nyoni

Tuesday May 12 2020

 

By EDO KUMWEMBE

KAMA tutaamua kuuamini mtandao wa Wikipedia basi Alhamisi hii iliyopita, Erasto Edward Nyoni ametimiza miaka 32. Kama tutaamua kuiamini pasipoti yake basi Erasto Edward Nyoni ametimiza miaka 32 Alhamisi hii.

Alizaliwa Mei 7, 1988. Umri umekwenda. Iwe amedanganya umri au hajadanganya umri bado umri wake umekwenda. Timu yake, Simba, wanahitaji mlinzi mwingine wa kati wa kuchukua nafasi yake. Iwe msimu huu au msimu ujao.

Erasto amekuwa mtamu zaidi uzeeni. Inasemwa hivyo kwake na kwa Kelvin Yondani. Pamoja na hilo lakini Erasto ataonekana mtamu zaidi katika soka la ndani. Soka la kimataifa, yeye pamoja na Serge Pascal Wawa wataonekana kutupwa na wakati.

Ilionekana katika michuano ya kimataifa msimu uliopita hasa wakati Simba ilipokuwa ugenini. Ni wachezaji wanaotumia akili zaidi lakini suala la kasi ni suala la umri. Imekuwa hivi ukimchunguza Erasto. Ana akili nyingi za soka lakini hana kasi sana.

Tumgeukie Erasto. Kuna maswali ya kujiuliza baada ya juzi kutimiza miaka 32. Hivi kwanini wachezaji wetu wanakuwa watamu zaidi uzeeni? Takwimu nyingi zinawabeba zaidi magolikipa kwamba wanapozeeka wanacheza vizuri zaidi. Kwanini sisi hadithi inakuwa tofauti? Kwanini wachezaji wanaoonekana kuwa wakubwa ndio wanakuwa wazuri zaidi?

Kuna Kelvin, Erasto, na sasa pia tuna Abdulhalim Humud. Kwanini wamekuwa watamu uzeeni? Unatamani kwamba mpira ambao Erasto anacheza sasa angekuwa anacheza hivyo akiwa na umri wa miaka 23. Mbona wakati huo hatukumjua?

Advertisement

Jibu la kwanza ni kwamba kina Erasto wamefikia kilele cha ubora wao baada ya kukusanya uzoefu kwa miaka mingi. Uzoefu huu ni mechi za kimataifa akiwa na Azam, Simba na Taifa Stars. Kwanini wenzetu wengine wanaweza kukomaa wakiwa na miaka 20 tu?

Kuna jibu moja. Wenzetu wamewekeza sana katika soka la vijana. Katika umri mdogo wanacheza mechi nyingi za kuwafanya wapevuke haraka. Kwa mfano, nyuma ya pazia, akiwa na umri wa miaka 17 tu, mchezaji kama Kylian Mbappe utakuta alishiriki katika michuano ya vijana katika michuano mbalimbali ambayo haimo hata katika ratiba ya FIFA au UEFA.

Unaweza kukuta Mbappe na makinda wenzake wa umri wake walishawahi kucheza michuano mbalimbali ya vijana katika nchi zaidi ya 10 Ulaya. Ni rahisi kwake kukomaa akiwa kinda. Tanzania soka la vijana halina mechi nyingi za ndani wala za nje. Mchezaji anakutana na mechi nyingi akiwa na umri mkubwa.

Upevukaji (maturity) kwa wachezaji wa Tanzania unachelewa. Achilia mbali upevukaji wa mwili lakini upevukaji wa akili pia unachelewa. Mwisho wa siku mchezaji kama Erasto alipaswa kutuonyesha anachotuonyesha akiwa na umri wa miaka 19. Na kama angetuonyesha kitu hicho akiwa na umri huo leo Erasto angekuwa anacheza Marseille au Borussia Dortmund.

Kitu kingine ambacho kilimficha Erasto ni kucheza Azam. Tuna matatizo katika macho yetu pindi mchezaji anapocheza Azam au Prisons. Matatizo hayo ya macho huwa yanamalizika pindi mchezaji anaposaini Simba au Yanga.

Awali mchezaji hapati sifa anazostahili pindi anapocheza Azam. Zamani niliwahi kuandika mahala kuwa Erasto ni mchezaji aliyekuwa na akili kubwa ya mpira kuliko wote nchini. Hakuna aliyejali kwa sababu mchezaji mwenye akili kubwa ya soka nchini lazima atoke Simba au Yanga.

Mpira huu ambao Erasto anaucheza sasa ameucheza muda mrefu akiwa na Azam. Sifa anapata zaidi sasa hivi akiwa na Simba. Na hata makocha wa timu ya taifa wanapata shinikizo kubwa la kupanga vikosi ambavyo vina wachezaji wa Simba na Yanga.

Mtazame huyu Aishi Manula. Akiwa na Azam kulikuwa hakuna matatizo yoyote kuhusu uwezo wake. Leo mashabiki wa Simba wanalalamika kwamba Aishi anafungwa mabao ya mbali. Hawatoi mifano ya wakati anacheza Azam au wakati anacheza Taifa Stars kabla hajajiunga na Simba.

Wachezaji wazuri wanaocheza timu za mikoani wakati mwingine tunawachelewesha bila ya sababu za msingi. Mfano mzuri ni Godfrey Bony. Bila ya Marcio Maximo sidhani kama angekuja Yanga. Alimuona kule Prisons akamuita timu ya taifa. Ghafla Yanga ikamsajili na kila mtu akawa anaimba kipaji chake. Kabla ya hapo? Hakukuwa na hadithi hiyo.

Hii ina maana kama ni kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi basi Bony angeenda kwa sababu ya kuonwa akiwa na Yanga na si Prisons.

Hili ni tatizo la msingi ambalo linasababisha wachezaji wafike kiwango cha juu wakiwa na umri mkubwa.

Na ndicho ambacho kimemtokea Erasto. Na sasa Simba ijipange kumchukua mchezaji mwingine wa kuziba nafasi ya Erasto. Miguu itasaliti kasi yake muda mchache ujao. Kwa Ligi yetu anaweza kuendelea kuwa bora lakini Simba ina mipango mikubwa nje ya Ligi yetu na simuoni Erasto katika mipango hiyo.

Timu ya taifa pia inahitaji mlinzi mwingine wa kati. Bahati mbaya kwa timu ya taifa kama ilivyo Simba nao wanahitaji walinzi wawili wapya wa nafasi ya kati kwa sababu Kelvin na Agrey Morris wanaondoka. Simba wanaweza kwenda nje na kuchukua walinzi wa kuziba nafasi za Nyoni na Wawa, lakini taifa haliwezi kwenda nje.

Birthday za wachezaji kama kina Erasto zinatia uchungu. Sio kitu cha kufurahisha. Kama hii hapa iliyopita ya Erasto imezidi kumpeleka Erasto katika uzee huku tukiwa hatuna jina la mbadala wake.

Labda tuone kama Bakari Mwamnyeto anaweza kufikia mambo ambayo wakubwa wenzake wamefanya.

Haya, Mwamnyeto na nani?

Advertisement