Guardiola atengeneza timu mbili zote moto unaambiwa

Muktasari:

  • Kama wakali hao akiwanasa, basi Guardiola atakuwa na vikosi viwili matata sana kwenye ligi hiyo msimu ujao.

MANCHESTER, ENGLAND.PEP Guardiola anajiandaa kuwa na vikosi viwili matata vya Manchester City atakavyotamba navyo msimu ujao ambapo vimedaiwa kuwa na thamani ya Pauni 855 milioni.
Kwa msimu ujao, Man City itakuwa bize kufukuzia taji lake la tatu mfululizo kwenye Ligi Kuu England huku wakisaka pia ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ripoti zilizopo ni kwamba Man City imepanga kufanya usajili wa mastaa watatu matata kabisa katika dirisha hili la majira ya kiangazi na tayari wameripotiwa kukubali kulipa Pauni 62.5 milioni kunasa kiungo wa kati wa Atletico Madrid, Rodri.
Ada hiyo itaweka rekodi huko Etihad, kwa sababu mchezaji ambaye amesajiliwa kwa pesa nyingi zaidi katika timu hiyo ni Riyad Mahrez, Pauni 60 milioni. Guardiola pia anamtaka beki wa kati Harry Maguire na anamfukuzia beki wa kulia, Joao Cancelo. Kama wakali hao akiwanasa, basi Guardiola atakuwa na vikosi viwili matata sana kwenye ligi hiyo msimu ujao.
Kikosi cha kwanza, golini atakuwa Ederson (Pauni 35milioni), wakati mabeki wake ni Benjamin Mandy (Pauni 52m), Aymeric Laporte (Pauni 57m), John Stones (Pauni 47.5m) na Kyle Walker (Pauni 45m), huku kwenye kiungo kutakuwa na David Silva (Pauni 24m), Fernandinho (Pauni 30m) na Kevin De Bruyne (Pauni 55m), wakati kwenye fowadi kutakuwa na wakali watatu Leroy Sane (Pauni 37m), Raheem Sterling (Pauni 49m) na Sergio Aguero (Pauni 38m) na kufanya kikosi hicho kuwa na thamani ya Pauni 469.5 milioni.
Kikosi cha pili, golini ni Claudio Bravo (Pauni 15.4milioni), mabeki wake ni Zinchenko (Pauni 1m), Maguire (Pauni 80m), Nicolas Otamendi (Pauni 32m) na Cancelo (Pauni 45m), wakati kwenye viungo watatu watakuwa na Ilkay Gundogan (Pauni 20m), Rodri (Pauni 62.5m), Foden (kutoka kwenye akademia), wakati kwenye fowadi kutakuwa na Bernardo Silva (Pauni 43m), Mahrez (Pauni 60m) na Gabriel Jesus (Pauni 27m) na kufanya kikosi hicho kuwa na thamani ya Pauni 385.9 milioni.