‘Goli’ la Samatta gumzo kila kona

Muktasari:

Hadi mapumziko, KRC Genk walienda vyumbani wakiwa nyumba kwa bao 1-0 na mambo yaliwaendea kombo kipindi cha pili kwa kuongezwa mengine matatu licha ya kupata moja la kufutia machozi kupitia kwa Odey.

NYOTA wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga Genk KRC, hana hamu na teknolojia baada ya usiku wa kuamkia jana kumtibulia kuandika rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kufunga bao dhidi ya klabu kubwa barani Ulaya, Liverpool ya England katika mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Teknolojia ya usaidizi wa video kwa waamuzi ‘VAR’, ilizima ndoto ya nahodha wa timu ya taifa, Taifa Stars kuifunga Liverpool kwenye mchezo wa kwanza kukutana na miamba hiyo ya soka, England hatua ya makundi baada ya bao lake la kichwa la dakika ya 27 kukataliwa na mwamuzi kwa kutumia VAR.

Samatta alifunga bao, ambalo lingekuwa la kusawazisha kwa kichwa katika kipindi hicho cha kwanza, lakini mwamuzi Slavko Vincic aliomba usaidizi wa VAR. Baada ya kutazamwa bao lile la Samatta, Mslovenia ambaye alikuwa akichezesha mchezo huo, alilikataa kitu kilichozaa mijadala kwa waliokuwa wakiufuatilia mchezo huo na hasa Watanzania waliokuwa wakiutazama kupitia vibanda umiza mbalimbali.

Wapo waliodhani kukataliwa kwa bao la Samatta kulitokana na kumtumia kwake James Milner kama ngazi kabla ya kufunga, huku wengine wakiona tukio lile huenda alikuwa kwenye eneo la kuotea.

Hadi mapumziko, KRC Genk walienda vyumbani wakiwa nyumba kwa bao 1-0 na mambo yaliwaendea kombo kipindi cha pili kwa kuongezwa mengine matatu licha ya kupata moja la kufutia machozi kupitia kwa Odey.

Mabao mengine ya Liverpool kwenye mchezo huo, yalifungwa na Oxlade-Chamberlain kwa mara nyingine tena huku, Sadio Mane na Mohammed Salah kila mmoja akifunga moja.

SAMATTA AMWIBUA LINEKER

Mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya England, klabu ya Barcelona, Gary Lineker ameshangazwa na uamuzi wa kukataliwa kwa bao la Samatta katika mchezo huo wa Jumatano.

Lineker aliyekuwa mchambuzi katika mchezo huo aliandika katika ukurasa wake wa Twitter@GaryLineker What Samatta with that? na kupata Retweets zaidi ya 474 na Likes zaidi ya 4.5K pamoja na maoni zaidi ya 394 kutoka kwa watu mbalimbali wanaofuata katika mtandao huo. Baada ya kukataliwa kwa bao hilo mashabiki wa Genk 20, 000 waliokuwa kwenye Uwanja wa Luminus walisikika wakipiga kelele kwa kumzomea mwamuzi kwa kukataa bao hilo.

MSIKIE MWENYEWE

Samatta alisema uzoefu wa Liverpool katika ligi hiyo ilikuwa moja ya sababu za wao kupoteza mchezo huo licha ya kucheza kama timu.

“Tulijiandaa kucheza kama timu lakini mambo hayakuwa mazuri upande wetu. Kuna muda unatakiwa kujifunza kutokana na kile ambacho kimetokea. Nina imani tutasimama upya na kwenda kupigania matokeo ya ushindi Anfield,” alisema nahodha huyo na kuligusia bao lake lililokataliwa kwa kusema;

“Nilitamani kufunga ndiyo maana nilipopata ile nafasi nilishangilia kwa nguvu kwa sababu niliona nimeikomboa timu yangu, baada ya kukataliwa niliumia, lakini nilijipa moyo naweza kufunga tena na kwa bahati mbaya haikuwezekana.” Samatta mwenye bao moja katika mashindano hayo, alipachika bao lililokataliwa dhidi ya Liverpool baada ya kubainika alizidi kabla ya kupigiwa krosi, aliyoimalizia kwa kichwa mbele ya James Milner.

Kwa matokeo ya jumla kwenye kundi lao, E, wanaoongoza ni Napoli wenye pointi saba, wanaofuata Liverpool (6), Salsburg (4), Genk (1).

NYOTA NAO WAZUNGUMZA

Beki wa Kagera Sugar, David Luhende alisema Samatta ametambulisha ulimwengu anaweza akacheza popote.

“Samatta ametoa funzo kwetu inawezekana penye nia na kufanya juhudi, si jambo la kitoto kukabana na Van Dijk beki mahiri ambaye alichukua tuzo ya dunia, kaipeleka Tanzania mbali na anaweza akacheza klabu yoyote Ulaya, ameidhihirishia dunia.”

“Sijui kwa nini walilikataa bao lake, ingawa Genk na Liverpool ni vitu viwili tofauti kabisa ila yeye kucheza kwa kiwango anastahili pongezi na kuigwa na chipukizi wanaokuja nyuma,” alisema.

Straika wa Ruvu Shooting, Christopher Edward naye aliitazama mechi hiyo na kusema; “Kafanya kitu kikubwa kinastahili pongezi na kimetoa somo mchezaji akijituma inawezekana akaonyesha maajabu, nina imani atacheza klabu kubwa Ulaya.”

Naye Khamis Mcha ‘Vialli’ anayecheza Dodoma FC alisema; “Ameonyesha kiwango cha hali ya juu ninachoamini kitampa dili la kucheza Ulaya kama tulivyokuwa tunasikia tetesi za kwenda huku, ametupa funzo la kujituma na kuheshimu kazi.”

Kiungo wa Yanga Fesal Salum ‘Fei Toto’ alisema amejifunza mengi juu ya kuishi kwa malengo kupitia mchezo huo wa Samatta dhidi ya Liverpool.

“Kwanza nasema lile kwangu lilikuwa bao mimi nahesabu Genk walipata mabao mawili,lakini kiukweli Sammata amenifundisha kuishi na malengo naamini alikuwa na ndoto na akaamua kuishi nazo kwa ukweli na kuweka juhudi,” alisema Fei Toto