Fei Toto, Gadiel wabakizwa Dar

Muktasari:

Baada ya Yanga jana kupoteza mchezo wa pili katika ligi ikiwa imetoka sare mara nne inaendelea kumpa mwanya Simba kutetea ubingwa wake wanaoendelea kuushikilia baada ya kutwaa msimu uliopita kama wataweza kupata matokeo katika michezo yake yote ya vipolo.

KIKOSI cha wachezaji 20 wa Yanga wanatarajiwa kupaa kwa ndege leo Jumatatu kuifuata Mbao FC, lakini ikiwaacha nyota wake wawili, kiungo Feisal Salum 'Fei Toto' na beki Gadiel Michael ambao wataukosa mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Mechi hiyo ngumu imekuja siku chache Yanga ikitoka kupoteza mchezo wao dhidi ya Simba uliopigwa juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa na kupunguzwa kasi yao ya kukusanya pointi ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo inayoingia raundi ya 28.
Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh alisema kikosi kinatarajia kuondoka asubuhi ya leo kikiwa na nyota 20 tu huku Fei Toto na Gadiel wakiachwa kwa vile wana kadi tatu za njano zinazowazuia kukipiga kwenye mchezo huo, huku wakiwa na kumbukumbu ya kulala 2-0 jijini Mwanza katika mechi yao ya mwisho na Mbao kukutana jijini humo.
Hafidh alisema maandalizi yao yameenda sawa wanachokisubiri ni safari tu, huku akisisitiza wamsahau matokeo yao na Simba na kuangalia namna ya kulipa kisasi kwa Mbao wakiwa kwao kwani mara nyingine imekuwa ikiwatoa nishai Kirumba.
"Nyota tunaoondoka nao ni, Ramadhani Kabwili, Paul Godfrey, Haji Mwinyi, Andrew Vincent, Kelvin Yondani, Abdallah Shaibu, Mohammed Issa, Papy Tshishimbi, Heritier Makambo, Amissi Tambwe, Ibrahim Ajibu, Klaus Kindoki, Juma Abdul, Haruna Moshi 'Boban', Mrisho Ngassa, Matheo Anthony, Deus Kaseke, Raphael Daud, Jaffar Mohammed na Said Makapu," alisema.