Eymael awavulia kofia Simba SC

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Luc Eymael amewapongeza Simba kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimamu wa tatu mfululizo.

Simba wametwaa ubingwa huo jana baada ya sare ya 0-0 ugenini Mbeya na kufikisha pointi 79 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine huku raundi sita za mechi zikisalia ili ligi kumalizika.

Eymael alisema Simba wanastahili kupongezwa kwa sababu wametwaa ubingwa wa ligi. Hongera kwao kwa kuwa mabingwa. Macho yetu yanapaswa kuangalia msimu ujao, kilichopo kwa sasa ni kuhakikisha tumaliza katika nafasi hii ya pili.

“Ni ngumu kumaliza nafasi ya pili kutokana na ushindani uliopo lakini nina imani na wachezaji wangu kuwa watapigania hii nafasi kwa ajili ya kumaliza msimu kwa heshima. Kuna muda inabidi ukubaliane na mazingira,” alisema.

Yanga ilipanda hadi nafasi ya pili kwa kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Ndanda juzi Jumamosi, shukrani kwa mabao ya Deus Kaseke na mtokea benchini, Mrisho Ngassa waliosaidia kupindua meza baada ya Yanga kutanguliwa kwa mabao 2-1.

Mabao ya Ndanda yalifungwa na Abdul Seleman na Omary Mponda.

Azam ilishikiliwa katika sare ya 1-1 dhidi ya Biashara Mara na kuachia nafasi ya pili kwa Yanga katika msimamo.

Kabla ya kuendelea na michezo ya Ligi Kuu Bara, Yanga watakuwa na kibarua kizito kesho Jumanne cha kulipa kisasi cha kupigwa 3-0 dhidi ya Kagera Sugar katika mechi yao iliyopita ya Ligi Kuu Bara wakati timu hizo mbili zitakapokutana katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho.

Mechi nyingine ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho kesho ni kati ya Namungo na Alliance wakati keshokutwa Jumatano Simba watacheza dhidi ya Azam FC, huku pia Sahare All Stars ikwakabili Ndanda.