Eymael aimaliza Simba kijanja

Muktasari:

Simba na Yanga zinakutana Jumapili ijayo kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA ambayo ndiyo iliyoshikilia hatma ya Yanga kimataifa msimu ujao.

YANGA ina mechi mbili ngumu za Ligi Kuu Bara ugenini dhidi ya Biashara United leo na Kagera Sugar itakayopigwa Alhamisi, lakini Kocha wao Luc Eymael mjanja sana. Hajali sana hizo mechi. Akili yake iko kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kukipiga na watani zao, Simba.

Simba na Yanga zinakutana Jumapili ijayo kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA ambayo ndiyo iliyoshikilia hatma ya Yanga kimataifa msimu ujao.

Luc ameliambia Mwanaspoti kwamba pamoja na changamoto za mechi ya leo, lakini akili yake inaicheza kimbinu mechi ya Simba ambayo ndiyo iliyoshikilia heshima yao kwa sasa.

“Kwa sasa tuna mechi za Ligi Kuu, lakini tunacheza pia mchezo wetu muhimu na Simba ambao, utatupa matumaini ya kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani,” alisema Eymael ambaye Mwanaspoti linajua kwamba ameshazungumza na makocha wenzake kadhaa walioko Afrika Kusini na Ubelgiji wamsaidie pia kuusoma mchezo huo kimbinu ndani ya uwanja.

Kocha huyo alisisitiza kwamba mchezo huo wana kila sababu ya kuucheza vizuri na kupata matokeo kwa kuwa, ni kazi ya dakika 90 tu tofauti na ligi ambayo bado inaendelea.

Awali, Luc aliiambia Mwanaspoti kwamba timu yake inahitaji kushiriki kwa namna yoyote ile mashindano ya kimataifa msimu ujao kwani, mastaa wengi wapya wa kigeni anaotaka kuwasajili wamezoea kushiriki michuano mikubwa hivyo, itakuwa rahisi kuwapata.

DHIDI YA BIASHARA

Licha ya kwamba Yanga haina rekodi ya kupata matokeo mazuri dhidi ya Biashara hasa mjini Musoma, Luc amelalamikia uchakavu wa Uwanja wa Karume.

“Nimeiandaa vizuri timu kupata matokeo lakini uwanja tunaocheza sio rafiki kabisa, huwezi kucheza mechi nzuri yenye mbinu, lazima kubutuabutua na kupiga mipira mbele ili kupata matokeo. Timu kubwa na yenye mashabiki wengi kama Yanga inapaswa kucheza kwenye uwanja mzuri,” alisema.

“Lazima tubadilishe hivi viwanja kama tunataka kuimarisha soka la klabu hata kuwa na timu nzuri ya Taifa ambayo inaweza kushindana sehemu kama Tunisia,” aliongeza.

Mara ya mwisho kukutana timu hizo kwenye Uwanja wa Karume, Yanga ikiwa chini ya Kocha Mwinyi Zahera ililala bao 1-0.

Hadi sasa Yanga wamekusanya pointi 60 huku Biashara ikiwa nafasi ya tisa kwa alama 44 baada ya timu zote kushuka uwanjani mara 32.

“Kikosi changu kipo vizuri licha ya baadhi ya wachezaji kama Benard Morison na Papy Tshishimbi kutokuwapo lakini tunatarajia matokeo mazuri, hatuwadharau wapinzani,” alisema.

Naye Kocha Mkuu wa Biashara United, Francis Baraza alisema hana wasiwasi na mchezo huo kwani, wamefanya maandalizi ya kutosha na mkakati wao ni kubaki na alama tatu muhimu.

“Sisi tunawasubiri uwanjani, hatuna presha na nimewaandaa vyema vijana wangu kuhakikisha tunabaki na pointi tatu ili kujiweka pazuri kwenye msimamo,” alisema Kocha huyo raia wa Kenya.

Baraza anayeoonekana mbabe kwenye mechi zao za nyumbani, alisema malengo yao ni kumaliza katika nafasi tano za juu hivyo lazima wapambane katika mechi sita zilizobaki ili wafanye vizuri.

Kwa sasa Biashara ipo nafasi ya tisa katika msimamo ikiwa na pointi 44, baada ya kucheza michezo 32, imeshinda 11, imetoka sare michezo 11 na kupoteza 10 na Baraza alisema licha ya kuiheshimu Yanga kama timu kubwa yenye wachezaji wazuri lakini hawaihofii.

Alisema mbinu walizotumia kuidhibiti Azam waliotoka nao sare ya 1-1, ndio watakayoitumia mechi dhidi ya Yanga.

“Ukiangalia mechi iliyopita dhidi ya Azam ilikuwa nzuri na tukiweza kurudisha bao na kumaliza mchezo kwa sare ya bao 1-1. Walikuja na mfumo wa kujilinda zaidi,” alisema Baraza.

Tangu Baraza atue ndani ya Biashara, Novemba mwaka jana timu hiyo haijawahi kupoteza mchezo wowote wa ligi nyumbani, na imecheza mechi 11 na kushinda tisa huku ikitoka sare mbili, ilihali kwa mechi za ugenini pia amecheza mechi 11, akipata sare saba na kupoteza nne.

Pia rekodi inaonyesha kwenye mechi za jumla za Biashara United kwa msimu huu nyumbani imecheza 14 na kushinda 11, ikipoteza miwili na kutoka sare moja.