Domayo atuliza mashabiki Azam

Muktasari:

Azam ambao walipata nafasi hiyo baada ya kutwaa kombe la FA, watawakabali  Jumapili, Fasil Kenema S.C ambao walimaliza nafasi ya tatu kwenye Ligi ya Ethiopia msimu uliopita.

KIUNGO  wa Azam,  Frank  Domayo ‘Chumvi’ amesema hesabu zao ni kuanza vizuri mchezo wa ugenini wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Fasil Kenema ya Ethiopia  watakaocheza nao kesho Jumapili ili wasiwe na presha kubwa katika mechi ya marudiano.
Chumvi ambaye ni sehemu ya wachezaji wa Azam waliosafari kwa kwenda  Ethiopia na kufikia katika hoteli ya Solyana, iliyopo Bahir Dar, alisema kwenye mashindano ya kimataifa kuna faida muda mwingine kuanzia ugenini.
Kiungo huyo wa zamani wa Yanga, alisema faida iliyopo ni kujitengenezea mapema uwezekano wa kusonga mbele kama yatapatikana matokeo mazuri kwao.
“Kucheza ugenini kunahitaji utulivu siku zote kwa sababu wenyeji wanakuwa na faida ya kuwa nyumbani. Tulipata maandalizi katika mashindano haya kupitia kombe la Kagame ni matumaini yangu kuona tunafanya vizuri,” alisema Domayo.
Naye kiungo chipukizi kwenye kikosi hicho, Masoud  Abdallah ‘Cabaye’  alisema malengo yao ni kuhakikisha wanatinga hatua ya makundi ya kombe la shirikisho ili wailetee heshima Tanzania.
“Nadhani hiki ni kipindi cha timu za Tanzania kufanya vizuri, tunakazi kubwa mbele yetu lakini hakuna kinachoshindikana penye nia na dhamira ya kweli,” alisema  Cabaye.
Mara  ya mwisho kwa Azam, kushiriki kombe la shirikisho ilikuwa Machi 19, 2017 ambapo waliondolewa katika raundi ya kwanza kwa jumla ya mabao 3-1 na Mbabane Swallows ya Eswatini, katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam, waliibuka na ushindi wa bao 1-0, walipoenda ugenini waliruhusu mabao 3-0.