Dilunga, Ambokile wamsema Makambo

Muktasari:

Achana na vita ya msimamo wa Ligi Kuu Bara ambayo Simba na Azam FC wanaifukuzia Yanga inayomiliki pointi 50 katika mechi 18, sasa ni Haritie Makambo, Said Dilunga na Eliud Ambokile.

BAADA ya straika wa Yanga, Heritier Makambo kuongoza kwa mabao 11, Said Dilunga (Ruvu Shooting) anayemiliki mabao 10 na Eliud Ambokile (Mbeya City) tisa, wamemwandalia mkakati maalumu wa kuhakikisha wanampindua.
Dilunga ambaye ameweka wazi hana malengo ya kuchukua kiatu cha dhahabu badala yake anataka kiende kwa Eliud Ambokile ameapa kumng'oa Makambo nafasi aliopo.
"Kanza nataka nianze na kuvunja rekodi anayoishikiria mchezaji mwenzangu kwenye timu, Abdulrahman Mussa walioiweka na Simon Msuva akiwa Yanga, msimu wa 2016/17 kabla hajaenda Morocco,"alisema Dilunga.
"Baada ya kukamilisha hilo ndipo nitaanza kufikiria ndoto nyingine mbele ya safari, kiukweli natamani Ambokile awe mfungaji bora msimu huu kwani anajua kucheka na nyavu na hatuwezi kumpa nafasi Makambo ya kuwa chini yake, tutapambana kadri tuwezavyo,"anasema.
Kwa upande wa Ambokile anasema amejipanga kuweka ushindani dhidi ya mastaa wa Simba na Yanga ambao wanaonekana kuwa na kibali mbele ya jamii ya soka nchini.
"Yanga wana kitu kimoja cha kuhakikisha kila kitu wapo juu kama kwenye msimamo wa ligi hata mfungaji na wanapata nguvu ya mashabiki, lakini kwa vyovyote vile sitarudi nyuma kufikia malengo yangu katika msimu huu.
"Kubwa zaidi ikitokea mimi nikakosa kiatu cha dhahabu basi achukue mzawa yeyote ili tuvunje rekodi ya Msuva na mchezaji ambaye namwona anaweza akafanya hivyo ni Said Dilunga wa Ruvu,"anasema.