Betty: Dawa ya kumtuliza Mkwassa hii hapa-2

Betty Mkwassa ambaye ni mke wa nyota na nahodha wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Charles Boniface Mkwassa katika mahojiano na gazeti hili ameeleza namna walivyokutana hadi kuanzisha mahusiano yao yaliyozaa ndoa iliyodumu kwa miaka 30 sasa.

Katika mwendelezo wa makala ya Betty anaeleza namna alivyoweza kumtuliza stress za uwanjani Mkwassa ambaye anasisitiza alikuwa mlevi wa mpira na aliumizwa mno pale timu yake inapopata matokeo mabaya.

“Japo tulikubaliana stress za uwanjani mwisho ni getini ndani hakuna kuingia nazo, lakini Mkwassa alikuwa mlevi wa mpira, hivyo kuna wakati anajitahidi kutoonyesha tofauti baada ya matokeo mabaya, lakini alishindwa na kuna wakati alikuwa mnyonge.

Anasema mtu uliyemzoea mara zote anapokuwa tofauti utajua tu na ndivyo ilikuwa kwake na Mkwassa ambaye timu yake ilipokuwa ikifungwa japo alijitahidi kutoonyesha tofauti akifika nyumbani ila aliishia kunyong’onyea.

“Nyumbani tuko wanne, mimi yeye na watoto wetu wawili tumezoea kutaniana, hivyo wakati mwingine watoto wako shule, tunabaki wawili, akifungwa huko pamoja na kwamba tumeshakubaliana mambo ya mpira yanaishia getini, bado alikuwa akionyesha kunyong’onyea licha ya kujitaidi kuficha hisia zake, lakini nilikuwa nafahamu.

“Nilichokuwa nafanya nampikia chakula anachokipenda, hii ilikuwa dawa yake, Mkwassa anapenda kula ugali, samaki na mlenda pamoja na mtindi, hivyo akifika mezani stress zote zinakwisha, nikimwona amenyong’onyea basi nampikia chakula anachopenda anafurahi maisha yanaendelea,” anasema.

Anasema katika mambo ambayo yalikuwa yakimuuzi ni utamaduni wa Mkwassa kutowapiga watoto tangu wameoana mwaka 1989 na kubahatika kupata watoto wawili lakini hajawahi kumpiga mtoto wake yoyote mpaka sasa.

“Nilikuwa nakasirika, alikuwa tofauti na mimi kwani mimi mtoto akikosea namlapua kwanza ndipo namuuliza, lakini Mkwassa ni tofauti sijui kwa vile ana chembechembe za ualimu, kwake mtoto akikosea anakaa chini na kuongea naye kwa kumwelekeza, hajawahi kupiga mtoto tangu amenioa.

Anasema katika maisha yao ya ndoa amewahi kumwona Mkwassa akikasirika na kufikia hatua ya kutaka kupigana mara moja tena akiwa uwanjani na si nyumbani.

Betty anasema siku hiyo alishangazwa na mwonekano wa Mkwassa, hakuamini kilichotokea kwani hakuwahi kuona katika hali ile.

Akikumbuka tukio lile, Betty anasema: “ilikuwa zamu yangu kusoma taarifa ya habari, wakati ule ukiwa zamu unasoma habari zote hadi za michezo zile za uwanjani zilikuwa zinachelewa, hivyo zililetwa tayari nikiwa studio na moja ya habari ilikuwa ya Mkwassa akiwa kocha wa Sigara.

“Nilipoisoma naona video inamwonyesha amekasirika kweli kweli amenyanyuka kwenda kumvaa refa, nikabaki napigwa na butwaa, badala ya kusoma habari nikajikuta nasema kwa nguvu eeeh huyu vipi, kwani imekuwaje? wakati niko hewani.

“Ni kitu ambacho kilinishangaza, sababu sikuwahi kumwona Mkwassa amekasirika namna ile, niliporudi nyumbani nikamuuliza, lakini watu walitutania kweli mimi na yeye, siwezi kusahau tukio lile,” alisimulia Betty huku akicheka.

Wawili hao ambao wameanza urafiki mwaka 1983 kabla ya kufunga ndoa mwaka 1989 wanapenda kufanya mazoezi pamoja kila siku Asubuhi kabla ya majukumu ya kazi.

“Nafikiri mazoezi kwa asilimia kubwa ndiyo yamechangia hata niwe fiti na afya ya Mkwassa iimarike kwa haraka baada ya kufanyiwa upasuaji India,” anasema Betty.

Alikuwa katika mazingira gani baada ya mmewe kuugua?

Betty anasema kilikuwa kipindi kigumu kwa familia, hakuna kilichofanyika zaidi ya kuhakikisha afya ya mmewe inaimarika na kuacha kila kitu ikiwamo kujiuzuru kuongoza klabu ya Yanga.

Alivyojiuzulu Yanga mambo yalikuwaje?

Tukio ambalo Wanachama na mashabiki wa Yanga hawatolisahau ni kujiuzuru kwa Mkwassa nafasi ya katibu Mkuu, ilikuwa ni jambo la ghafla ambalo hakuna aliyejua sababu za nahodha na kocha huyo wa zamani wa Yanga kujiuzulu.

Mkwassa alikuwa amekaa madarakani kwa miezi 17 tangu alipongazwa katibu mkuu wa klabu hiyo kongwe Janauari 31, 2017.

Wapo waliodhani amezinguana na Mwenyekiti, Yusuph Manji, pia wapo waliodhani zengwe ndani ya klabu hiyo limemshinda ndiyo sababu kaamua kuondoka na wengine waliamini amelazimishwa kujiuzulu, kila mmoja alisema alivyoweza.

“Ilikuwa ni jambo ambalo liliacha ahueni kwa familia,” anasema Betty huku Mkwassa akibainisha Mungu ndiye alimwongoza ajiuzuru kwani alijiona mwepesi mara tu baada ya kutangaza maamuzi hayo.

“Nilikuwa kwenye kipindi kigumu wakati niko Yanga, kuna wakati ilifika nikawa napoteza kumbukumbu, kama nilitaka kujibu au kuandika barua fulani ya klabu, najikuta ghafla tu nimesahau nilichotaka kufanya, naweza nikakumbuka siku inayofuata,” anasimulia.

Mkwasa anasema, kipindi hicho alikuwa anachoka sana, alihisi labda ni sababu ya umri, pia alikuwa akihisi joto kupita kiasi na wakati mwingine alihisi baridi kali mno, akadhani hali ya hewa ya Dar es Salaam.

“Siku moja tulikuwa kanisani, wakati tumesimama kuimba, nilishindwa, mwili uliishiwa nguvu, Bety mke wangu alikuwa jirani, aliniambia kaa chini usisimame, nikafanya hivyo hadi ibada ilipokwisha, tukaondoka.

“Nilienda na Betty tukapima kwenye moja ya hospitali za binafsi, nikaambiwa na tatizo kwenye moyo, nikampingia simu profesa Mohamed Janabi (Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete), yule ni family friend wetu tangu zamani.

Mkwasa anasema, akiwa katika harakati za kuhakikisha afya yake inaimarika, alikaa na kufikiria na familia yake, akaona wakati muafaka wa yeye kuondoka Yanga ili aangalie kwanza afya yake.

“Nilifikiria kuomba likizo ya ugonjwa, lakini nikaona hiyo itasababisha watu kuongea maneno maneno, nikaona bora niondoke moja kwa moja kwenye masuala ya mpira, nipumzike.

“Nilikaa mwenyewe, hakuna aliyenishauri niandike barua, nilifanya uamuzi binafsi nikiwa na familia yangu tu,” anasema.

Anasema baada ya kuandika barua ya kujiuzuru, kwa kiasi fulani aliona kama ametua mzigo kichwani, hakujua ni kwa sababu gani lakini tangu pale alijiona ametua mzigo, alihisi kupata faraja kwa kiasi fulani.

“Nilimpigia simu profesa Janabi, aliniuliza hali yangu nikamueleza profesa Leo nahisi kama kichwa changu chepesi, akaniuliza kwa nini nikamueleza kuwa ni baada ya kujiuzulu kuwa katibu mkuu wa Yanga, Profesa akaniambia, umefanya jambo la busara huo ni mzigo namba moja umeutua, hongera kwa uamuzi uliochukua.

Baada ya kuachana na Yanga, ikafuata ishu ya matibabu na Betty anajua alipambanaje kuhakikisha mumewe anakuwa sawa. Endelea nayo tena kesho Jumatatu kujua mengi zaidi.