Corona kushusha bei ya Sancho

Thursday May 21 2020

 

DORTMUND, UJERUMANI. BOSI wa Borussia Dortmund, Carsten Cramer amesema kuna uwezekano mkubwa wakaamua kushusha bei ya staa wao, Jadon Sancho kutokana na janga la corona.

Staa huyo Mwingereza mwenye umri wa miaka 20 amekuwa mmoja wa wachezaji gumzo kabisa huko Ulaya kwa sasa kutokana na soka lake la kiwango cha juu analolicheza katika kikosi cha Borussia Dortmund huko kwenye Bundesliga.

Kutokana na hilo, klabu kadhaa vigogo huko Ulaya wamekuwa wakihaha kupata saini yake huku Manchester United wakiripotiwa kuongoza kwenye mbio za kuwania huduma ya mshambuliaji huyo.

Dortmund awali ilikuwa imeng’ang’ania kwenye bei yake ya awali, kwamba Sancho wanamuuza Pauni 120 milioni, lakini Cramer ameibuka na kusema klabu hiyo ya Ujerumani inapaswa kuwa na mawazo tofauti na kufikiria upya hasa kutokana na janga la corona lilivyoathiri uchumi wa klabu nyingi huko Ulaya.

“Kawaida wakati kama huu kila mwaka vikosi vya msimu ujao vinakuwa vimeshapatikana. Pengine unaweza kuuza wachezaji, lakini mipango inakuwa imeshakabilika,” alisema Cramer.

“Kwa sasa kila mtu ameamua kubadilika kwa kadri anavyoweza. Nina uhakika biashara za mikopo zitakuwa kubwa kuliko muda wote na watu hawatakuwa na muda wa kutosha kuandaa mipango kwenye vikosi vyao.

Advertisement

“Nina uhakika mkubwa, si Julai Mosi wala Agosti Mosi timu zitakuwa zimeshajiandaa. Utulivu mkubwa unahitajika. Nina uhakika hata yale matarajio ya kuuza mchezaji kwa pesa kubwa yatashuka pia.”

Sancho, ambaye ana mkataba Dortmund hadi 2022, amefunga mabao 17 na kuasisti mara 19 kwenye michuano yote aliyochezea kikosi hicho kinachonolewa na kocha Lucien Favre msimu huu.

Advertisement