Conte kumbeba jumla Sanchez

Sunday May 31 2020

 

MILAN ITALIA. INTER Milan imethibitisha kwamba supastaa Alexis Sanchez ataendelea kubaki kwenye kikosi chao hadi mwisho wa msimu huu wakipiga hesabu za kunasa jumla huduma ya mkali huyo aendelee kukipiga kwenye Serie A.

Fowadi huyo wa Manchester United, Sanchez amekuwa kwa mkopo kwenye kikosi cha miamba hiyo ya Serie A tangu kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana na alipaswa kurejea Old Trafford mwezi ujao.

Mikikimikiki ya Serie A ilisimama kutokana na janga la corona, hivyo jambo hilo lingemfanya Sanchez kuachana na timu hiyo ya San Siro kabla ya msimu kumalizika kwa sababu mkataba wa mkopo utakuwa umefika mwisho.

Lakini, kurugenzi wa michezo wa Inter Milan, Piero Ausillo alisema staa huyo wa zamani wa Arsenal atapewa nafasi ya kuthibitisha uwezo wake kwamba anastahili kuongezewa muda zaidi wa kucheza kwenye timu hiyo baada ya msimu huu kumalizika. Serie A inatarajia kurejea upya Juni 20, huku mechi zake zikiripotiwa zitachezwa bila ya mashabiki.

Majeruhi yamemtibulia Sanchez huko Italia, ambapo ameishia kufunga mabao moja tu katika mechi 15 alizochezea kikosi hicho kinachonolewa na kocha Antonio Conte. Lakini, Ausillo alisema kuhusu Sanchez: “Ataendeelea kubaki hapa hadi mwisho wa msimu na baada ya hapo tujadili hatima yake na Manchester United. Hii ni nafasi kwake ya kutuonyesha uwezo wake.” Kama Sanchez atashindwa kunasa dili la kudumu Inter, basi kinachoripotiwa kwamba huenda akarudi kwao Chile baada ya maisha yake kuwa magumu Old Trafford. Kwa kufunga mabao 43 katika mechi 132, Sanchez ni shujaa mkubwa huko kwao Chile.

Advertisement