Bocco, Kapombe, Mkude wamenoga kwelikweli

SIMBA jana imeendelea na mazeozi yake kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena uliopo Bunju B kando kidogo ya jiji la Dar es Salaam lakini nyota nane katika mazoezi hayo walionekana kunoga zaidi na kutengewa mazoezi yao.

Kikosi hicho chini ya kocha wao Sven Vandenbroeck ambaye amekalia kuti kavu la kuendelea kuinoa timu, kilianza mazoezi yake saa 2 hadi saa 4 asubuhi.

Sven aliwanoa wachezaji kwa mazoezi ya kuchezea mpira, kupigiana pasi na baadaye aliwagawa wachezaji wake katika makundi mawili ambapo baadhi walisimamiwa na yeye pamoja na msaidizi wake Seleman Matola.

Wachezaji waliokuwa chini yake akiwemo kinara wa mabao Mnyarwanda Meddie Kagere waliendelea na mazoezi ya kukimbia pembezoni mwa uwanja huo huko wale nane walioonekana kuwa fiti wakiwa chini ya kocha wa viungo Adel Zrane.

Nyota hao waliofuzu vyema mtihani wa kwanza wa Sven waliongozwa na nahodha wao John Bocco, Erasto Nyoni, Deo Kanda, Shomari Kapombe, Yassin Mzamiru, Paschal Wawa, Jonas Mkude na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Mazoezi hayo waliyokuwa wanafanya wachezaji nane yalikuwa ni ya kuruka koni yaliyofanyika kwenye uwanja wa nyasi bandia huku wale wengine wakibaki kwenye uwanja wa nyasi asilia.

Wakati mazoezi hayo yanaendelea ilielezwa kuwa kocha aliwatenga nyota hao kwa vile ameona wameweza kwenda vizuri na programu yake ya kipindi chote walichokaa nyumbani kutokana na ufiti walionao.

Akizungumza mara baada ya mazoezi hayo, Bocco alisema mazoezi ya siku tatu yamewapa mwanga namna gani ligi ikianza itakavyokuwa ngumu ambapo wao wamebakiwa na mechi 10 huku wakiongoza ligi kwa pointi 71.

“Tumepumzika kwa kipindi kirefu, lakini jambo zuri ni kwamba makocha walitupa programu kipindi tupo nyumbani na wote tulizifuata kwa sababu hata siku hizi tatu kocha ametupa mazoezi ya kutupima kama kweli tulikuwa tunafuata programu zake na tunashukuru tumeweza kumridhisha kuwa hatukuwa tunakaa tu bali tulikuwa tunafanya mazoezi.

“Malengo yetu bado ni yale yale kushinda mechi zetu zote ziliobaki na kutwaa ubingwa na hicho ndicho tunachotarajia kufanya na tunaomba Mungu atusaidie, ingawa ligi ikiendelea inaonekana itakuwa ngumu zaidi ya mwanzo kwani timu zinapambana kutoshuka daraja,” alisema Bocco

Shiboub, Chama na Kahata

Kuhusu kutokuwepo kwa nyota wake Clatous Chama, Sharaf Shiboub na Francis Kahata, Sven alifafanua kwamba Chama na Kahata wanaweza kurejea nchini mwanzoni mwa wiki ijayo lakini changamoto ipo kwa Shiboub kutoka Sudan.

“Sudan marufuku yao ina mkazo sana katika kipindi hiki cha corona lakini Kenya na Zambia walau kuna nafuu, tunawategemea Chama na Kahata kuungana nao wiki ijayo,” alisema kocha huyo mwenye miaka 40.

Kuhusu viwango vya utimamu wa wachezaji wake, alisema sio mbaya licha ya kuwa kila mmoja alikuwa akifanya mazoezi binafsi akiwa nyumbani.

“Kibaya ni kuwa hatujui tutacheza lini mchezo wetu wa kwanza hivyo ni ngumu kupanga ratiba zetu ipasavyo za kujiandaa, lakini kila kitu naamini kitaenda vizuri,” alisema.

Simba kwa sasa mazoezi yao yatakuwa yakifanyika asubuhi na jioni tofauti na siku mbili za mwanzo ambapo walifanya mara moja.