Bergkamp afichua Wenger alivyotibua

LONDON ENGLAND. STAA wa zamani wa Arsenal, Dennis Bergkamp amefichua mabadiliko aliyofanya kocha Arsene Wenger kwenye kikosi hicho na kuwagharimu kiasi kikubwa hadi sasa.

Arsenal ilikuwa moto sana mwishoni mwa miaka ya tisini na mwanzoni mwa miaka ya 2000, ambapo walishinda mataji matatu ya Ligi Kuu England wakitumia fomesheni ya 4-4-2.

Katika mtindo huo wa kuichezaji, Bergkamp alipangwa Namba 10, akicheza nyuma ya washambuliaji Nicolas Anelka kisha Thierry Henry, alipotengeneza kombinesheni matata kabisa na Wafaransa hao.

Lakini, Wenger aliamua kuibwaga fomesheni hiyo iliyowaletea mafanikio makubwa sana hata kucheza ule msimu wa 2003/04 bila ya kupoteza kwenye ligi na mabadiliko aliyofanya ndicho kitu kilichokuja kuiharibu Arsenal.

Badala yake, Wenger aliamua kutumia mshambuliaji mmoja na kuongeza mtu wa ziada kwenye kiungo.

Na Bergkamp anaamini kitendo cha Arsenal kushindwa kuwania mataji baada ya yeye kuandoka mwaka 2006 kulichangiwa zaidi na mabadiliko hayo ya kimfumo katika uchezaji.

Bergkamp aliulizwa na mchezaji wa zamani wa Arsenal, Martin Keown kwanini miaka ya mwisho ya Wenger ilikuwa haina mafanikio, alijibu hivi: “Arsene alianza kufanya majaribio.

“Arsenal baada ya mwaka 2006, walikuwa wakicheza sana sehemu ya kiungo. Walikuwa hawana mchezaji wa kwenda mbele kushambulia, walitumia mshambuliaji mmoja tu, ambaye alikuwa mpweke.”

Keown alikubaliana na maneno ya mchezaji mwenzake wa zamani na kueleza kwamba kuondoka kwa Bergkamp kulimfanya Wenger aanze kumtumia Cesc Fabregas, lakini hakuwa kwenye namba 10 zaidi na alishambulia kutokea nyuma, ili kufanya kiungo kuwa na wachezaji wengi jambo ambalo liliigharimu sana timu na kukosa makali yake ya zamani.

Arsenal ilifika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2006, lakini wakachapwa na Barcelona na huo ndio ulikuwa mchezo wa mwisho wa Bergkamp katika kikosi hicho.

Baada ya hapo, mafanikio ya Arsenal ilikuwa kushinda Kombe la FA tu, walilobeba mwaka 2014 na kurudia 2015 na 2017 kabla ya Wenger kung’oka mwaka 2018.