Alphonso: Mkimbizi anakimbiza balaa Bayern Munich

MUNICH UJERUMANI. MAISHA yanahitaji kitu gani kingine zaidi ya maajabu yake.

Ushafikiria ule msemo wa kulala maskini na kuamka tajiri? Basi hicho ndicho kinachotokea kwa kinda mmoja anayekipiga katika kikosi cha Bayern Munich.

Kinda hiyo amekuwa na stori tamu ya maisha yake na sasa anatesa kwenye Bundesliga akiwa na kikosi cha Bayern Munich, huku Chelsea ikiwa moja ya timu iliyokiona cha moto kutoka kwake. Ushamjua? Wanamwita Alphonso Davies.

Majina yake halisi, ni Alphonso Boyle Davies, alizaliwa Novemba 2, 2000 huko Buduburam, Ghana. Davies anamudu kucheza winga, beki wa kushoto na wing-back.

Azaliwa kambi ya wakimbizi

Davies alizaliwa Buduburam, kambi ya wakimbizi iliyopo kwenye wilaya ya Gomoa huo Ghana. Wazazi wake ni raia wa Liberia. Wazazi wake walikimbia vita ya wenyewe kwa wenyewe huko Liberia, ambayo ilisababisha zaidi ya watu 450,000 kukimbia makazi yao. Wakati Davies akiwa na umri wa miaka mitano, familia yake ilihamia Canada na kwenda kuishi Edmonton. Juni 6, 2017 alipata uraia wa Canada.

Aibukia kwenye soka, atesa MSL

Baada ya kuzichezea Edmonton Internationals na Edmonton Skrikers, Davies alinaswa na Whitecaps FC Redsidency mwaka 2015 akiwa na umri wa miaka 14. Kisha akatua Vancouver Whitecaps FC wakati ilipokuwa ikijiandaa na msimu wa MSL mwaka 2016. Kipindi hicho aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kucheza kwenye ile ligi ya USL, miaka 15 na miezi mitano. Baada ya kuonyesha kiwango kikubwa katika timu ya watoto, Davies akaanza kuichezea timu ya wakubwa ya timu hiyo na kuonyesha kiwango bora kabisa. Akiwa hapo, akaanza kutesa kwenye MSL na kuzifanya klabu kibao za Ulaya kuanza kufukuzia saini yake.

Vigogo wamtaka, Bayern wanamnasa

Ubora wake wa uwanjani ulizifanya klabu kibao za Ulaya kuanza kumfukuzia. Kwenye Ligi Kuu England, Manchester United, Chelsea na Liverpool zikionyesha dhamira ya dhati ya kunasa saini yake, lakini Bayern Munich ndio waliofanikiwa kumsajili, wakitoa Pauni 17 milioni kwenye dirisha la Januari mwaka huu. Hiyo ni pesa nyingi zaidi kulipiwa mchezaji wa kutoka MLS. Pesa hiyo ilionekana kutumika vizuri baada ya Davies kuonyesha kiwango moto sana wakati Bayern ilipoichapa Chelsea 3-0 jkwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, mwezi Februari katika kipute kilichofanyika Stamford Bridge. Kiwango chake kiliwaamsha mastaa kibao kuanza kumzungumzia akiwamo Thomas Muller na Owen Hargreaves.

Ujio wa Davies kwenye kikosi hicho cha Bayern Munich kinawafanya kuamizi kwamba wameshapata mrithi wa kudumu wa David Alaba kutokana na uwezo wake wa kucheza kwenye beki ya kushoto, huku akiwa na uwezo mkubwa wa kushambulia.

Soka la kimataifa

Baada ya wazazi wake kukimbia vita huko Liberia. Davies hakutaka kurudi nyuma kwenda kuchagua kuichezea timu ya taifa ya nchi hiyo na badala yake amechagua kuiwakilisha Canada katika soka la kimataifa. Davies aligundua kuwa na kipaji cha soka na kuamua kujikita kwenye mchezo huo badala ya kushika bunduki kitu kilichokuwa kikifanya hata na watoto wadogo huko Liberia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe. Kipindi hicho hakuweza kupelekwa shule kwa sababu familia haikuwa na uwezo wa kifedha huku wakati mwingine ilishindikana hadi kupata nauli tu za kwenda kwenye mechi.

Lakini, baada ya kuonyesha ubora mkubwa kwenye kikosi cha Whitecaps, Wacanada hawakuwa na uamuzi mwingine zaidi ya kumpa uraia na sasa anacheza kwenye timu yao. Baada ya kutamba kwenye timu ya vijana, Juni 6, 2017 alipandishwa kwenye kikosi cha wakubwa cha Canada.

Na tangu wakati huo, Davies ambaye ni mpenzi wa staa wa kike wa soka wa Canada, Jordyn Huitema panga pangua amekuwa akiichezea Canada katika soka la kimataifa ikiwamo kwenye michuano ya CONCACAF Gold Cup na CONCACAF Nations League A.