Adeyun bado kidogo tu Oman

Dar es Salaam. Dili la kutakiwa na timu ya Nadi Oman na Seeb za Oman, limeanza kuonyesha dalili za mafanikio kwa beki wa Yanga, Adeyun Saleh.

Mpango huo umekuja baada ya kumpata meneja wa kusimamia kazi zake, Peter Simon ambaye ameingia naye mkataba wa miaka miwili.

Adeyun ameliambia Mwananchi kwamba bado ana mkataba na Yanga, lakini anaamini mpango wake ukienda vizuri, atakaa mezani na uongozi wa timu yake.

Adeyun ambaye alisajiliwa na Yanga katika dirisha dogo, akitokea JKT Tanzania alisema ni ndoto ya kila mchezaji kucheza nje ya mipaka ya nchi yake.

“Ndio maana natamani dili hilo litimie ili kukamilisha ndoto yangu baada ya kutumika ligi kuu nikiwa katika timu tofauti. Natamani nikapate changamoto nje lakini kwa kuzingatia taratibu zinazotakiwa kutoka Yanga.”

Alisema nje ya hizo timu, anaamini meneja wake ataendelea kusaka mipango mingine itakayomfanya kazi yake ifike mbali kama ilivyo kwa mastaa wengine kama Mbwana Samatta anayecheza Aston Villa ya England.

“Inawezekana nisifike kiwango chake lakini nikafanya katika nafasi yangu na fungu ambalo Mwenyezi Mungu amenipangia,” alisema Adeyun.