Madee hataki gharama, 700 tu inamtosha

Friday July 12 2019

 

By Rhobi Chacha

MWIMBAJI  wa muziki wa kizazi kipya, Hamad Ally ‘Madee’ ameweka wazi bajeti ya kila siku asubuhi kuwa ni Sh 700 na kwamba anafurahia maisha anayoishi uswahilini kwao.
Madee ambaye anaishi Manzese jijini Dar es Salaam amesema wasanii wengi wanatamani kuishi maisha hayo lakini wanashindwa kutokana na jinsi walivyojiweka.
Akifafanua pesa hiyo inavyotumika, Madee amesema ananunua vipande vinne vya muhogo wa kukaanga ambavyo vinagharimu Sh 400 pamoja na kikombe cha chai kinachouzwa Sh 300.
Madee amezungumzia suala la umaarufu na kusema maisha ya kuwa maarufu ni magumu sana kwani kuna wakati unashindwa kufanya vitu ambavyo wanavipenda kutokana na umaarufu wao.
Amesema kuna baadhi ya watu wanajutia maamuzi yao ya umaarufu kwani yanawafanya waishi maisha ambayo si yao kwani wakifanya vitu vingine baadaye vinageuka stori mitaani na mitandaoni.
"Maisha ninayoishi nyumbani kwangu Manzese huwa nayafurahia sana, ni maisha ya uswahilini kwa mtu ambaye ana umaarufu hawawezi kuishi, kuna wakati huwa nasema kwanini watu walitaka kuwa mastaa kwa sababu kuna wakati mwingine unatamani kufanya jambo fulani lakini unashindwa kufanya kutokana na umaarufu wako, maisha ya umaarufu magumu bora nibaki kuishi uswahili kwangu na vyakula vyangu vya bei poa," anasema MadeeAdvertisement