Lukaku afunguka kuhusu Man United

Muktasari:

Na sasa akiwa ameshafunga mabao tisa kwenye Serie A, straika huyo mwenye umri wa miaka 26 alisema alitambua nyakati zake za kuwa Old Trafford zimefika kikomo baada ya kubadilishwa nafasi ya kucheza na kupelekwa pembeni.

MILAN, ITALIA . STRAIKA, Romelu Lukaku amesema kwamba ametambua nyakati zake za kubaki Manchester United zimefika kikomo baada ya kocha Ole Gunnar Solskjaer kuanza kumchezesha winga.
Staa huyo wa kimataifa wa Ubelgiji, Lukaku alihamishiwa pembenni na kocha Solskjaer baada ya kutua tu Man United kuchukua mikoba ya Jose Mourinho, Desemba mwaka jana.
Alicheza kwenye winga Januari katika mechi ya Kombe la FA dhidi ya Arsenal na kucheza eneo hilo kwenye mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Liverpool uliopigwa Februari na hapo, Marcus Rashford alihamishiwa kati.
Lukaku alifunga mabao tisa chini ya Solskjaer,  huku mabao sita akifunga kwenye ligi kabla ya kutimkia zake Inter Milan kwa ada ya Pauni 74 milioni katika dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.
Na sasa akiwa ameshafunga mabao tisa kwenye Serie A, straika huyo mwenye umri wa miaka 26 alisema alitambua nyakati zake za kuwa Old Trafford zimefika kikomo baada ya kubadilishwa nafasi ya kucheza na kupelekwa pembeni.
"Baada ya kutambua tu kwamba Ole Gunnar Solsjkaer amepanga kunichezesha winga, nilifahamu kwamba wakati wangu wa kuwa Manchester United umefika mwisho," alisema Lukaku.
Kwa wakati huo, Lukaku hakuonyesha kitu chochote na kusema hajali apangwe kushoto au kulia kikubwa ni heshima tu anayopewa kuichezea timu hiyo, kwamba atafanya vizuri kwenye nafasi yoyote ile atakayopangwa.
Huko Inter, Lukaku amekwenda kuchukua nafasi ya Mauro Icardi, ambaye amepelekwa kwa mkopo PSG.