‘Kiwewe’ mechi na Yanga chatibua mapokezi Simba

Dar es Salaam. Mabingwa wa Ligi Kuu, Simba, waliwasili Dar es Salaam saa 2:40 asubuhi jana, wakitokea Ruangwa mkoani Lindi walikotoa suluhu na Namungo FC.

Baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakiwa na kombe la ubingwa huo, walikaa ndani ya jengo uwanjani hapo kwa dakika 40 kukiwa na vikao ambavyo havikuwa rasmi vilivyofanyika ili kumtuliza Kocha Sven Vandenbroeck ambaye alionekana kuwa mkali akizungumza kwa sauti ya juu huku akiwa amekasirika.

Katika vikao hivyo, Sven hakukubaliana na lolote ambalo aliambiwa na kaimu mwenyekiti wa Simba, Mwina Kaduguda, wasaidizi wa benchi la ufundi pamoja na wachezaji, na kuamua kutoka nje ya uwanja huku akiwa na hasira na hata wengi wa mashabiki waliojitokeza kumshangilia na kumpigia makofi hakuwa na habari nao.

Baada ya kutoka, Sven alianza kujibizana na msaidizi wa ofisa mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Rispa Hatibu akihoji kwa nini aliweka utaratibu wa wachezaji kupanda gari la wazi, huku akiacha wingi wa mashabiki kufika uwanjani hapo kuwapokea na kuwashangilia, jambo ambalo hakupenda akisisitiza wachezaji wakapumzike kujiandaa na mechi dhidi ya Yanga, Jumapili.

“Sitaki kuona mchezaji yeyote anapanda katika gari la wazi na kuzunguka nalo, badala yake wote wapande basi la timu na kwenda kambini moja kwa moja,” alisikika Sven akimueleza Rispa kwa ukali na sauti ya juu, ingawa naye wakati mwingi alikuwa akiwasiliana kwa simu, lakini haikufahamika nini alichokuwa akizungumza.

“Sitaki jambo lolote lifanyike hapa, hakuna mchezaji wala msaidizi wangu kufuata utaratibu ambao umepangwa, na nimewakataza kuzungumza hata na vyombo vya habari, tuna mechi ngumu ambayo tunahitaji utulivu tujipange kwa ushindi, hatuwezi kupoteza muda na nguvu,” alisikika Sven akiwaambia wenzake kwenye ‘mzozo’ huo.

Kwa upande wake, Rispa ambaye alikuwa akijibu huku machozi yakimlenga alieleza kuwa amefuata utaratibu ambao uliwekwa na uongozi na alikwenda uwanjani hapo kusimamia na kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri, na ndio maana walikodi na magari. “Unanikaripia mbele za watu ili iweje wakati ambacho nakifanya na mambo mengine ni masuala ambayo yalipangwa na uongozi, ambalo nalifanya ni utekelezaji wa majukumu yangu,” Rispa alijibu kwa sauti kali, huku akirusha mikono na wenzake wakijaribu kumtuliza.

Wakati mzozo huo ukiendelea kocha msaidizi, Selemani Matola na meneja wa timu, Patrick Rweyemamu waliingilia kati kuwatenganisha na kila mmoja alipelekwa upande tofauti ili kuepusha sintofahamu mbele ya mashabiki na wanahabari waliokuwepo.

Baada ya hapo wachezaji na benchi la ufundi walitoka ndani ya jengo la uwanja na kuingia katika gari ambazo zilifika kuwapokea na kwenda moja kwa moja kambini - Mbweni ambapo walisindikizwa na mabasi madogo matatu, magari madogo matatu na msafara wa bodaboda.

Mwananchi liliwafuata Kaduguda, Sven, Matola na Rweyemamu kuzungumzia mkanganyiko ulijiotokeza, lakini waligoma. Awali, mara baada ya mechi na Namungo FC kumalizika juzi, ofisa habari wa Simba, Haji Manara alieleza kwamba kikosi hicho kingewasili jana saa 3:30 asubuhi na baada ya hapo kingetumia gari la wazi ambalo lingewabeba wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi na baadhi ya viongozi wakiwa na kombe kuzunguka mitaani kuelekea makao makuu ya timu yaliyopo Msimbazi, kisha wangeelekea kambini.

Julio atoa neno

Akizungumzia sintofahamu iliyotokea, kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema: “Halikuwa jambo baya kutembea na kombe wakitokea uwanja wa ndege, lakini ni lazima uamuzi wa kocha uheshimiwe kwa sababu wachezaji wanatakiwa kuelekeza akili zao katika mchezo na Yanga kuliko sherehe za ubingwa.”

Imeandikwa na Thobias Sebastian, Oliver Albert na Eliya Solomon