Zidane aweka msimamo, Chelsea na PSG wapigwa chini
Muktasari:
- Zidane aliachana na Madrid mwaka 2021 na hadi sasa hana timu ingawa amekuwa akihusishwa na vigogo kibao Ulaya zikiwa timu za Taifa.
LONDON, ENGLAND: IMEFICHUKA. Baada ya Kocha Zinedine Zidane kuachana na Real Madrid, miamba ya England, Chelsea ilimfungia kazi kuipata huduma yake lakini akawakaushia.
Zidane aliachana na Madrid mwaka 2021 na hadi sasa hana timu ingawa amekuwa akihusishwa na vigogo kibao Ulaya zikiwa timu za Taifa.
Zidane anatarajiwa kwa kiasi kikubwa kuwa kocha ajaye wa Ufaransa akichukua mikoba ya Didier Deschamps baada ya Kombe la Dunia 2026.
Kwa mujibu wa AS, Chelsea ilifanya juhudi kubwa kumshawishi Zidane kwenda Stamford Bridge na inadaiwa klabu hiyo “ilimfuatilia kwa nguvu” ikimuona kama suluhisho la muda mrefu katika kipindi ambacho timu ilikuwa ikibadilisha makocha mara kwa mara.
Hata hivyo, licha ya pilika hizo mambo yalikuwa magumu kwani alipokea kila ujumbe kupitia kwa wakala wake na kuuweka kabatini kisha akanyamaza.
Wakati klabu mbalimbali Ulaya zikiendelea kumfuatilia, Zidane aliendelea kuwa na msimamo wa kusubiri kwa utulivu kuja kuifundisha nchi yake ambayo aliwahi kubeba nayo Kombe la Dunia.
Taarifa zinaonyesha amekuwa akiweka wazi anavutiwa na kazi mbili tu; kuinoa Ufaransa au kurejea Real Madrid na msimamo huo ndio uliofanya hata ofa kubwa kama ya Chelsea kushindwa kumshawishi.
Chelsea haikuwa klabu pekee iliyojaribu kumpata, kwani hata PSG na Al-Hilal ziliwahi kujaribu uwezekano wa kumchukua, huku Al-Hilal ikiripotiwa kumpa ofa kubwa zaidi.
Rekodi ya Zidane kama kocha inaendelea kuheshimiwa katika soka duniani, hususan alipokuwa Real Madrid alikoshinda mataji makubwa tisa, ikiwemo rekodi ya kushinda mara tatu mfululizo Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mafanikio hayo yanamuweka katika kundi dogo la makocha wanaoweza kusubiri nafasi bora badala ya kukubali kazi yoyote inayopatikana.
Kwa kuwa Deschamps anatarajiwa kuondoka baada ya Kombe la Dunia lijalo, njia ya Zidane kuinoa Ufaransa inaonekana kuwa wazi zaidi.