Xavi kupewa shavu jipya

BARCELONA, HISPANIA. MABOSI wa Ajax wanadaiwa kuanza mazungumzo na wawakilishi wa kocha wa Barcelona, Xavi kwa ajili ya kumpa shavu la kuifundisha timu hiyo baada ya kuondoka Barcelona mwisho wa msimu.

Ajax imekuwa na wakati mgumu kwa msimu huu ambapo hadi sasa inashikilia nafasi ya tano na ipo katika hatihati ya kufuzu michuano ya Ulaya kwa msimu ujao.

Imekuwa ikihusishwa na makocha wengi ambao ni Graham Potter na Erik ten Hag, lakini wote wameripotiwa kukataa na sasa wameamua kumgeukia Xavi ambaye ana mkataba na Barca hadi mwaka 2026.

Januari mwaka huu Xavi aliweka wazi kwamba ataondoka mwisho wa msimu huu akieleza sababu kubwa ni haoni kama anaheshimika.

"Kuna muda huwa unahisi kwamba unakosa heshima unayostahili na kazi unayofanya watu hawaithamini, hiyo inakufanya uharibike kisaiokolojia, mimi huwa ninapenda kuangalia mambo kwa jicho zuri lakini kila siku nazidi kuishiwa nguvu ya kuendelea kuitumikia timu hii, hadi hapa ilipofikia nafikiria hakuna haja ya kuendelea," alisema Xavi katika mahojiano yake wakati anatangaza kuondoka.

Mabosi wa Ajax wana matumaini makubwa ya Xavi kuifikisha timu hiyo katika nafasi nzuri kwa sababu hata falsafa za Barca hazitofautiani sana na zile za Ajax.
Pia kocha huyo tayari ameshaonyesha kwamba ana uwezo mkubwa wa kulea na kukuza wachezaji vijana kwani amefanya hivyo katika kikosi cha Barca ambapo amemuibua Lamine Yamal katika siku za hivi karibuni.

Ajax iliachana na kocha wao Maurice Steijn Oktoba mwaka jana baada ya kuiongoza timu hiyo katika mechi saba tu na kupata pointi tano.

Van 't Schip akapewa kibarua cha kuiongoza timu hiyo iliyokuwa nafasi ya 17 na baada ya hapo akapambana kuifikisha nafasi ya tano iliyopo sasa ambapo tofauti yao na timu iliyopo nafasi ya kufuzu Europa League ni pointi saba huku upande wa Ligi ya Mabingwa PSV na Feyenoord tayari zikionekana kufuzu.