Winga Cherki katua tunduni Man City

Muktasari:
- Staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 21 amesaini mkataba wa miaka mitano utakaomfanya adumu Etihad hadi 2030.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER City imethibitisha kumsajili kiungo wa Olympique Lyon, Rayan Cherki kwa ada ya Pauni 31 milioni.
Staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 21 amesaini mkataba wa miaka mitano utakaomfanya adumu Etihad hadi 2030.
Cherki anakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa na Man City kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya baada ya usajili wa Rayan Aït-Nouri na Marcus Bettinelli na kwamba ataruhusiwa kucheza kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu litakaloanza mwezi huu Marekani.
Cherki, ambaye aliichezea Lyon mechi 185, akifunga mabao 29 na asisti 45 alisema: “Hii ni ndoto kwangu. Ukweli, kujiunga na klabu kama Manchester City ni fursa ya kupiga hatua kubwa ya kwenye maendeleo ya soka langu, hii kitu ni spesho sana.
“Nimepambana sana kwenye maisha yangu yote. Naupenda huu mchezo, hivyo nasubiri kwa hamu kuboresha kiwango changu hapa Manchester chini ya kocha Pep na wasaidizi wake.
“Kila mtu anafahamu jinsi Man City ilivyo nzuri – imepata mafanikio kwa miaka mingi sana. Wajibu wangu ni kuisaidia timu kuendelea kushinda mataji. Naondoka Lyon kwa sababu ya imani ya mipango ya Man City kwamba itakwenda kuendeleza soka langu. Nataka kuwaonyesha mashabiki uwezo wangu.
Mkurugenzi wa soka wa Man City, Hugo Viana alisema: “Tumefurahi sana kwa kuwa na Rayan mahali hapa. Tunataka kuleta vipaji maridhawa kwenye hii klabu na yeye yupo kwenye kundi hilo.”