West Ham United yaacha watano, Antonio bado

Muktasari:
- West Ham ilithibitisha mwezi uliopita Lukasz Fabianski, Aaron Cresswell, Vladimir Coufal na Danny Ings wataondoka wakati mikataba yao itakapofika tamati Juni 30.
LONDON, ENGLAND: WEST Ham United imetangaza kuwatema wachezaji watano dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, lakini ikishindwa kubainisha chochote juu ya hatima ya straika wao, Michail Antonio.
West Ham ilithibitisha mwezi uliopita Lukasz Fabianski, Aaron Cresswell, Vladimir Coufal na Danny Ings wataondoka wakati mikataba yao itakapofika tamati Juni 30.
West Ham sasa imemwongeza Kurt Zouma kwenye orodha hiyo ya wachezaji watakaopatikana bure kabisa dirisha hili.
Antonio, ambaye alivunjika mguu kwenye ajali ya gari, Desemba mwaka jana, bado haelewi hatima ya maisha yake kwenye kikosi hicho cha London.
Taarifa ya klabu ya West Ham ilibainisha: “Hakuna uamuzi rasmi uliotangazwa kuhusu hatima yake hadi hapo muda mwafaka utakapofika.
“Hata hivyo, mkataba wake wa sasa utafika tamati Juni 30, kutokana na hilo la utaratibu wa Ligi Kuu England msimu wa 2024/25 unapofika mwisho, Michail ataorodheshwa kama mchezaji huru.”
Ripoti zinafichua West Ham na Antonio wamekuwa kwenye mazungumzo ya kuongeza mkataba, lakini bado hawajafikia makubaliano. Straika huyo mwenye umri wa miaka 35 aliposti video yake kwenye mtandao wa kijamii akionyesha jinsi anavyofanya mazoezi ya kutembea tangu alipopata ajali.
Straika huyo ni gwiji kwenye klabu ya West Ham, akiichezea mara 323 na kufunga mabao 83.