West Ham 2 Liverpool 2, ubingwa basi tena kwa Klopp

Muktasari:

  • TAKWIMU ZA MCHEZO
  • -Mashuti golini: West Ham 8, Liverpool 8
  • -Mashuti yote: West Ham 11, Liverpool 28
  • -Mashuti kuzuiwa: West Ham 1, Liverpool 6
  • -Umiliki mpira: West Ham 29%, Liverpool 76%
  • -Pasi zote: West Ham 266, Liverpool 669
  • -Pasi sahihi: West Ham 183, Liverpool 582
  • -Kucheza faulo: West Ham 8, Liverpool 10
  • -Kona: West Ham 4, Liverpool 8

LONDON, ENGLAND. LIVERPOOL imeishiwa pumzi kwenye mbio za kufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu na kurusha taulo baada ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya West Ham United, leo.

Na mwisho mbaya wa msimu wa Liverpool umehitimishwa na malumbano na staa Mohamed Salah na kocha wake Jurgen Klopp kabla ya staa huyo wa kimataifa wa Misri kuingia kwenye mechi hiyo.

Liverpool ilipaswa kushinda mchezo huo wa ugenini ili kuweka hai matumaini yao ya kunyakua ubingwa wa ligi msimu huu baada ya kutokea kuchapwa na Everton kwenye mechi iliyopita, lakini badala yake imepata sare, ambayo inawafanya kuzidiwa pointi mbili na vinara Arsenal, huku wakiwa wamecheza mechi moja zaidi.

Chama hilo la Klopp lilitokea nyuma na kuongoza mabao 2-1 kwenye kuelekea dakika za mwisho, lakini Michail Antonio alifunga kwa kichwa kuisawazishia West Ham ya kocha David Moyes na kufanya mechi kumalizika kwa sare hiyo ya mabao 2-2.

Matokeo hayo yanaifanya Liverpool kufikisha pointi 75 baada ya mechi 35. Kushinda ubingwa itawalazimu kuomba mabaya kwa Arsenal ipoteze mechi tatu kati ya nne ilizobaki, huku ikiomba pia, Manchester City ipoteze mechi nne kati ya tano ilizobakiza kitu ambacho ni kigumu na hivyo kutoa nafasi finyu sana kwa miamba hiyo ya Anfield kubeba ubingwa huo wa ligi msimu huu.

Katika mchezo huo, West Ham ilitangulia kufunga kwa bao la kichwa la Jarrod Bowen baada ya mpira wa kutenga kwenye kipindi cha kwanza, lakini Andy Robertson aliisawazishia Liverpool muda mfupi baada ya kuanza kipindi cha pili, kisha ikaongeza bao jingine baada ya kipa Alphonse Areola kujifunga.

Baada ya hapo ilikosa nafasi kadhaa za kufunga kabla ya West Ham kusawazisha kupitia kwa Antonio, aliyeunganisha vyema krosi ya Bowen.