Wenger: Shida ni ile sare

Muktasari:

  • Na kocha huyo wa zamani wa Arsenal mwenye heshima kubwa huko Emirates, alisema ile mechi ya sare ya bila kufungana baina ya Man City na The Gunners uwanjani Etihad ndiyo iliyobadili kila kitu kwenye mbio hizo.

LONDON, ENGLAND: Arsene Wenger amesema kitu kuhusu mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu zinazozihusisha klabu za Manchester City, Arsenal na Liverpool.

Na kocha huyo wa zamani wa Arsenal mwenye heshima kubwa huko Emirates, alisema ile mechi ya sare ya bila kufungana baina ya Man City na The Gunners uwanjani Etihad ndiyo iliyobadili kila kitu kwenye mbio hizo.

Wenger, ambaye aliongoza Arsenal kubeba mataji matatu ya Ligi Kuu England kwa miaka yake 22 aliyokuwa kocha wa kikosi hicho, alijaribu kuzungumzia mbio hizo za ubingwa wa msimu huu baada ya Washika Bunduki hao wa London kuonekana kama wanaweza kufanya jambo wakiwa chini ya Kocha Mikel Arteta, huku pia msimu uliopita, walikaribia.

Kabla ya mechi za wikiendi iliyopita, Arsenal ilikuwa kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, lakini kichapo kutoka kwa Aston Villa, huku Man City ikiichapa Luton Town, kulimfanya Pep Guardiola kumwengua msaidizi wake wa zamani Arteta kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo na kuweka pengo la pointi mbili.

Wenger alisema matokeo ya kufungwa na Aston Villa si chanzo cha kufanya Arsenal kuondoka kwenye mbio za ubingwa, bali ile sare ya bila kufungana uwanjani Etihad ndipo tatizo lilipoanzia.

Alisema vijana wa Arteta hawakuangalia umuhimu wa mechi hiyo na kusisitiza wangeshinda ingekuwa vizuri.

“Nilishangaa sana,” alisema Wenger baada ya mechi ya kichapo dhidi ya Aston Villa.

“Ni wazi unapocheza na timu bingwa kwao na huku mechi zikiwa zimebaki nane, unapaswa kutafuta nafasi ya kufanya mambo yawe tofauti, kama unaona fursa itumie. Arsenal ilipaswa kushinda ile mechi na nafasi hiyo ilikuwepo.

“Kilichonishangaza wikiendi iliyopita ni kuona Man City imepanda kileleni. Hakuna aliyetarajia hilo. Sawa inawezekana wapinzani wake mmoja ndiye angefanya vibaya, sio wote wawili. Hicho ndicho kinachoshangaza. Arsenal bado ina faida juu ya tofauti yake ya mabao.

“Hata kama Man City ingeshinda au kutoka sare, basi Arsenal ingekuwa juu yao, kama wangeshinda ile mechi ya Etihad. Zile zilikuwa pointi muhimu sana kwa sababu hata Man City hawakutengeneza nafasi nyingi.

“Napata hisia endapo kama wachezaji wa Arsenal wangejaribu kulazimisha, pointi tatu zilizokuwa zinapatikana. Unajua unapocheza na mpinzani wake mkubwa, ukipata nafasi ya kummaliza, mmalize.”

Kutokana na Arsenal kuwa nyuma kwa pointi mbili dhidi ya Man City huku kukiwa na mechi sita tu za kucheza, matumaini yao ya kumaliza ukame wa miaka 20 ya kunyakua taji la Ligi Kuu England yameanza kufifia.

Lakini, kocha Arteta alisema kwa kusisitiza anaamini kuna kitu kitatokea tu.

“Kuna uwezekano, huo ndio ukweli. Ilikuwa hivi miezi michache iliyopita, tunajua nyakati kama hizi zitakuja kutokea. Kwa sasa ni kupambana na kuamini kuna kitu kitakwenda kutokea,” alisema.