Wenger ameshtua watu Italia
Muktasari:
- Gwiji huyo wa Arsenal alikwenda kushuhudia mechi hiyo wakati Como iliposhinda 2-0, huku kikosi hicho kikinolewa na aliyekuwa mchezaji wake wa zamani, kiungo Cesc Fabregas.
ROME, ITALIA: MASHABIKI wa soka wamebaki kwenye mchangao mkubwa baada ya kumwona Arsene Wenger uwanjani kwenye mechi ya Como dhidi ya Juventus kwenye Serie A.
Gwiji huyo wa Arsenal alikwenda kushuhudia mechi hiyo wakati Como iliposhinda 2-0, huku kikosi hicho kikinolewa na aliyekuwa mchezaji wake wa zamani, kiungo Cesc Fabregas.
Wenger aliungana na Thierry Henry na Raphael Varane, huku wote wakiwa ni Wafaransa.
Como ipo kwenye kiwango bora kabisa Serie A na sasa ipo pointi moja tu pungufu ya kufikia nafasi ya kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Na jambo hilo ndilo linalofanya kuvutia wageni wenye umaarufu kama Wenger. Jukwaani, Wenger alikuwa sambamba na Henry, ambaye pia ni mwekezaji kwenye kikosi cha Como, sambamba na Fabregas. Wawili hao waliungana na beki wa zamani wa Manchester United na Real Madrid, Raphael Varane.
Varane alijiunga na Como baada ya kuondoka Old Trafford mwaka 2024, lakini alipata majeraha katika mechi yake ya kwanza na hivyo kuamua kustaafu. Mashabiki wa Como walishangaa kumwona Wenger uwanjani kwenye mechi yao.
Shabiki wa kwanza amesema: “Arsene Wenger na Henry walikuja kumwona Como. Wenger atakuwa anajivunia sana.”
Mwingine aliongeza: “Kumwona Arsene Wenger na Thierry Henry wakikaa pamoja inarudisha kumbukumbu nyingi. Ni watu wawili hatari.”
Shabiki wa tatu amesema: “Wenger na Henry, hiyo inaeleweka, lakini vipi kuhusu Varane?” Na shaiki wa nne amesema tu: “Wow.”