Guardiola kuwakutanisha mezani Ferguson, Wenger
Muktasari:
- Guardiola amepanga kufanya hivyo baada ya ushindi wa 1–0 ilioupata Manchester City dhidi ya Brentford hali iliyompa nafasi ya kujiunga na kundi la makocha wachache waliowahi kufikia rekodi hiyo wakiwa na klabu moja pekee.
Kufikisha ushindi wa 250 katika Ligi Kuu England ni mafanikio makubwa yanayohitaji aina maalum ya sherehe. Kupitia hilo, Pep Guardiola amepanga kuwakutanisha Sir Alex Ferguson na Arsene Wenger mezani kula chakula cha jioni pamoja.
Guardiola amepanga kufanya hivyo baada ya ushindi wa 1–0 ilioupata Manchester City dhidi ya Brentford hali iliyompa nafasi ya kujiunga na kundi la makocha wachache waliowahi kufikia rekodi hiyo wakiwa na klabu moja pekee.
Ni Sir Alex Ferguson (Manchester United) na Arsène Wenger (Arsenal) pekee waliowahi kufanya hivyo kabla yake na Guardiola tayari anapanga orodha ya wageni wa kusherehekea mafanikio hayo.
“Ni heshima kubwa kuwa sambamba na Sir Alex Ferguson na Arsène Wenger, nitawaalika wote kwenye chakula kizuri cha jioni,” amesema kocha huyo ambaye yuko katika msimu wake wa 10 akiwa na City.
“Ni furaha kuwa sehemu ya historia ya Ligi Kuu England, nimeridhika sana. Sasa twende kwa ushindi 250 zaidi.”
Guardiola amefanikisha hilo baada ya michezo 349 pekee ya ligi kuu, rekodi ya kasi zaidi, kwani amewazidi Ferguson (michezo 404) na Wenger (michezo 424).
Katika enzi ya Ligi Kuu England, David Moyes pia ana jumla ya ushindi 250, lakini ameyapata akiwa na klabu mbalimbali.
Guardiola amejiunga na orodha ya makocha wengine 16 waliowahi kufikia idadi hiyo katika historia ya ligi kuu ya England, wakiwemo Bill Shankly (Liverpool), Matt Busby (Manchester United) na Brian Clough (Nottingham Forest).