We ni refa? Msikie Pierluigi Collina
Muktasari:
- Ukiweka kando wachezaji na makocha, Mtaliano Collina ni mmoja wa sura maarufu kabisa kwenye mchezo wa soka. Licha ya kwamba aliachana na kipyenga mwaka 2005, mechi yake ya mwisho ya kiushindani ilikuwa ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Villarreal na Everton, bado amekuwa mtu muhimu kwenye mabadiliko ya mchezo wa soka kwa upande wa waamuzi.
ZURICH, USWISI: MWENYEKITI wa kamati ya waamuzi wa Shirikisho la kimataifa la soka (FIFA), Pierluigi Collina amefunguka marefa wazuri kwenye mchezo wa soka wana kazi kubwa ya kufanya uwanjani kama wanataka kufikia kiwango chake na kupata nafasi ya kuchezesha fainali za Kombe la Dunia.
Ukiweka kando wachezaji na makocha, Mtaliano Collina ni mmoja wa sura maarufu kabisa kwenye mchezo wa soka. Licha ya kwamba aliachana na kipyenga mwaka 2005, mechi yake ya mwisho ya kiushindani ilikuwa ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Villarreal na Everton, bado amekuwa mtu muhimu kwenye mabadiliko ya mchezo wa soka kwa upande wa waamuzi.
Collina alishuhudia uanzishwaji wa Video Assistant Referees (VAR) kutokana na kazi yake FIFA, na alihusika pia kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu wakati ilipoibuliwa sheria mpya ya kuwadhibiti makipa kukaa na mpira kwa sekunde nane.
Collina aliweka kumbukumbu za kipekee kwenye kazi yake ya urefa, alichezesha mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 1999 wakati Manchester United ilipofunga mara mbili kwenye dakika za majeruhi kupindua matokeo dhidi ya Bayern Munich na kunyakua mataji matatu mwaka huu, wakati alikuwa mwamuzi wa kati pia kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Dunia 2002, wakati Brazil ilipoichapa Ujerumani 2-0.
Collina, 65, wakati anafanya kazi hiyo aipendayo hakukuwa na mapinduzi ya usaidizi wa teknolojia na alianza miaka ya 1970 hadi sasa, akifanya kazi ofisini baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya waamuzi wa Fifa.
Collina alisema kwa sasa yeyote anayetaka kuwa mwamuzi mzuri basi anapaswa kuwa na ufahamu mkubwa wa kuhusu mchezo wa soka na si kufahamu tu sheria na kanuni na atahitaji kurudia mechi nyingi mara kwa mara ili kupata ufahamu zaidi wa kuhusu mchezo huo. Wakati alipoulizwa ni kitu gani waamuzi wengine wafanye kufuata nyayo zake, alisema: “Nadhani kitu muhimu ni kuwa na uelewa wa mchezo wa soka. Kulikuwa na zama za kwamba ukijua tu sheria na kanuni basi unaweza kuwa refa, lakini kwenye soka la kisasa, unahitaji kuufahamu vyema mchezo huo. Unapaswa kujiandaa vizuri. Unapaswa kufahamu kile kinachoweza kwenda kutokea kwenye uwanja wa mchezo. Unapaswa kusoma na kujifunza. Matayarisho ya mwamuzi yamekuwa mapana sana kwa sasa, sio kujua sheria tu, hivyo ndivyo soka la sasa linavyohitaji. Kuna matukio yanaweza kukupita ndani ya uwanja, hivyo unapaswa kuangalia tena marudio ya mchezo.”
Collina alizaliwa, Februari 13, 1960 huko Bologna, Italia. Alianza kazi ya urefa 1977, akichezesha kwenye ligi za Italia za Serie C1, C2, B, A na kuwa kwenye orodha wa waamuzi wenye beji ya FIFA kuanzia 1995 hadi 2005. Alichezesha mechi 240 za cSerie A na 109 za kimataifa.
Mechi kubwa zaidi alizowahi kuchezesha, fainali ya Olimpiki 1996, fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 1999 na fainali ya Kombe la Dunia 2002. Alichaguliwa kuwa refa bora wa dunia kwa miaka sita mfululizo 1998 hadi 2003 na alichaguliwa Italian Football Hall of Fame (2011) na alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa waamuzi wa Serie A kuanzia 2007 hadi 2010, Ofisa Mkuu wa Waamuzi na Mwenyekiti wa kamati ya waamuzi wa UEFA hadi 2018. Kwa sasa ni mwenyekiti wa kamati ya waamuzi wa FIFA.