WATAUANA: Vita ya top 5 England ni kukabana koo
Muktasari:
Ushindi wa Arsenal dhidi ya Sporting Lisbon Jumanne usiku uliifanya England kuendelea kupeleka timu tano Ligi ya Mabingwa Ulaya na msimu huu zilitinga sita baada ya Tottenham kubeba taji la Europa League na msimu ujao unasubiriwa kama Nottingham Forest itaongezeka katika idadi hiyo kwa kufanya maajabu ya kubeba taji hilo kwani iko nafasi ya 16 katika msimamo wa Ligi Kuu England.
LONDON, ENGLAND: VITA ya kuwania nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya itaondoka na kichwa cha mtu katika mikikimikiki ya Ligi Kuu England na miamba sita inakabana koo.
Uhakiwa wa kinara wa lii hiyo Arsenal na mpinzani wake wa nafasi ya pili, Manchester City kufuzu ni asilimia miamoja na miamba mingine Manchester United, Aston Villa, Liverpool, Chelsea, Brentford na Everton mtawalia, na zote zimebakiza mechi saba kumaliza msimu.
Ushindi wa Arsenal dhidi ya Sporting Lisbon Jumanne usiku uliifanya England kuendelea kupeleka timu tano Ligi ya Mabingwa Ulaya na msimu huu zilitinga sita baada ya Tottenham kubeba taji la Europa League na msimu ujao unasubiriwa kama Nottingham Forest itaongezeka katika idadi hiyo kwa kufanya maajabu ya kubeba taji hilo kwani iko nafasi ya 16 katika msimamo wa Ligi Kuu England.
Hata hivyo, kwa sasa katika msimamo zinaangaliwa timu sita zinazokabana koo kupata tatu zitakazoungana na Arsenal na Man City kwenye Ligi ya Mabingwa na vita inazidi kuwa kubwa kati yao.
MAN UNITED
Man United ya Kocha Michael Carrick ambayo tangu ajiunge nayo inaonekana kuleta mabadiliko makubwa, inakamatanafasi ya tatu na inahitaji ushindi wa mechi tatu tu kujihakikishia kufuzu katika michuano hiyo mikubwa Ulaya.
Mechi zilizosalia za Mashetani hao wekundu ni dhidi ya Leeds (Nyumbani), Chelsea (Ugenini), Brentford (Nyumbani), Liverpool (Nyumbani), Sunderland (Ugenini), Nottingham Forest (Nyumbani), na Brighton (Ugenini).
ASTON VILLA
Aston Villa ambayo inaweza kupenya katika michuano hiyo kwa namna mbili, kumaliza ndani ya top 5 au kubeba kombe la Europa League, kwa sasa inakamata nafasi ya nne katika msimamo wa ligi, ikiizidi Liverpool kwa pointi tano.
Kikosi hicho cha Kocha Unai Emery kimepitia wakati mgumu ikishinda mechi mbili tu kati ya nane za mwisho za ligi na imebakisha mechi dhidi ya Nottingham Forest (Ugenini), Sunderland (Nyumbani), Fulham (Ugenini), Tottenham (Nyumbani), Burnley (Ugenini), Liverpool (Nyumbani) na Man City (Ugenini).
LIVERPOOL
Liverpool ambayo msimu huu unaonekana kuwa mgumu kwao wakishindwa hata kutetea taji lao la Ligi Kuu kwa sasa wako nafasi ya tano kwenye msimamo na inatakiwa kupambana kusalia hapo.
Mechi zao saba zijazo ni dhidi ya Fulham (Nyumbani), Everton (Ugenini), Crystal Palace (Nyumbani), Man United (Ugenini), Chelsea (Nyumbani), Aston Villa (Ugenini) na Brentford (Nyumbani).
CHELSEA
Vita katika nafasi hiyo ya tano ni dhidi ya Chelsea iliyo nyuma kwa pointi moja na inatakiwa kupambana kuidondosha Liverpool. Msoimu huu umekuwa mgumu kwao hadi kumfukuza Kocha Enzo Maresca na kumwajiri Liam Rosenior na imetoka kupoteza mechi mbili za mwisho za EPL, jambo ambalo limepunguza kasi yao katika mbio zao za kufuzu Ligi ya Mabingwa.
Mechi zao saba zilizosalia ni pamoja na Man City (Nyumbani), Man United (Nyumbani), Brighton (Ugenini), Nottingham Forest (Nyumbani), Liverpool (Ugenini), Tottenham (Nyumbani) na Sunderland (Ugenini).
BRENTFORD
Wakati huo huo, mbali ya vigogo hao sita. Brentford pia ina nafasi ya kufuzu michuano hiyo ikiwa itaendelea kufanya vizuri ikiwa nafasi ya saba na ina tofauti ya alama tatu tu dhidi ya Liverpool iliyopo katika nafasi ya kufuzu michuani hiyo.
Mechi zake zilizosalia ni dhidi ya Everton (Nyumbani), Fulham (Nyumbani), Manchester United (Ugenini), West Ham United (Nyumbani), Manchester City (Ugenini), Crystal Palace (Nyumbani) na Liverpool (Ugenini)
EVERTON
Everton ya David Moyes ina nafasi ya kufuzu michuano hiyo na pengo la pointi zake na Liverpool ni tatu na inasubiriwa kuona itafanya nini katika mechi saba ilizosalia.
Jambo zuri kwao ni itakuwa na mechi dhidi ya wapinzani wao katika nafasi hiyo Brentford na Liverpool na ikiwa itashinda itakuwa imejisogeza mbele zaidi.
Mechi zao zilizobaki ni dhidi ya Brentford (Ugenini), Liverpool (Nyumbani), West Ham (Ugenini), Manchester City (Nyumbani), Crystal Palace (Ugenini), Sunderland (Nyumbani) na Tottenham (Ugenini).