Wapo vizuri! Carragher adai Arsenal watasumbua sana Top Four

Muktasari:

KILA mtu ana chaguo lake. Rio Ferdinand amesema sasa anashawishika kusema Manchester City wanabeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

LONDON, ENGLAND. KILA mtu ana chaguo lake. Rio Ferdinand amesema sasa anashawishika kusema Manchester City wanabeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Kabla ya hapo, chaguo la beki huyo wa kati wa zamani wa Manchester United kwenye mbio za ubingwa wa ligi lilikuwa Chelsea.

Kuna wanaoamini Manchester United inaweza kufanya maajabu sambamba na Liverpool kwenye mchakamchaka huo wa kusaka ubingwa wa England kwa msimu huu.

Lakini, beki wa kati wa zamani wa ligi hiyo aliyekuwa akikipiga Anfield, Jamie Carragher ameibuka na kusema hakika Arsenal ndiyo timu ya kuichunga zaidi msimu huu. Carragher anaamini Arsenal watafanya maajabu.

Arsenal haijapoteza mchezo katika mechi nne zilizopita kwenye Ligi Kuu England chini ya kocha wao Mikel Arteta na kugeuza kibao baada ya kuwa kwenye nafasi za chini kwenye msimamo wa ligi hiyo kwa mwezi Septemba.

Na gwiji huyo wa Liverpool, Carragher anaamini Arsenal watasumbua na kuzitikisa timu zilizopo kwenye Top Four kwa sasa, ambazo ni Manchester City, Liverpool, Chelsea na Manchester United.

Mechi nne bila ya kuruhusu bao katika mechi tano zilizopita walizocheza kwenye michuano yote, hiyo ina maana kwamba chama hilo la Arteta sasa limeanza kurudi kwenye ubora wake, tofauti na ilivyokuwa mwanzoni mwa msimu ambapo iliruhusu wavu wake kuguswa mara tisa katika mechi tatu za kwanza kwenye Ligi Kuu England. Carragher anaamini Arsenal watasumbua.

Hata hivyo, Carragher, 43, anaamini haitakuwa kazi nyepesi kwa Arsenal kwa sababu Chelsea, Liverpool, Man City na Man United kila moja itahitaji kuwamo kwenye Top Four ili kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Akiandika kwenye kolamu yake ndani ya gazeti la Telegraph, Carragher alisema hivi: “Tunaweza kuona tayari Top Four ina timu zenye nguvu zaidi kwenye Ligi Kuu England.”

Lakini, aliendelea kwa kusema: “Lakini, timu ambayo nadhani inastahili kutazamwa zaidi msimu huu ni Arsenal.

“Kama wataendelea kupata matokeo haya chanya kwenye kikosi chao chenye vijana wengi na hawana presha ya mechi za michuano ya Ulaya, hilo litakuwa na msaada mkubwa sana kwa kocha Mikel Arteta kwa sababu amekuwa na muda mwingi wa kuwa na wachezaji wake mazozini.

“Bado mapema kuwafikiria watafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, lakini nadhani watakuwa moja ya watu watakaochuana kwenye hilo kwa sababu wana kikosi kizuri cha kushindana.”

Tofauti na ilivyo kwa Chelsea, Liverpool na klabu mbili za Manchester, Arsenal hawana msongamano wa ratiba kwa sababu hawapo kwenye michuano yoyote ya Ulaya msimu huu.

Washiriki wengine kwenye kufukuzia nafasi ndani ya Top Four, Tottenham, Leicester City na West Ham United wao wanakabiliwa na ratiba ngumu, wakiwa na mechi za ligi za ndani na michuano ya Ulaya.

Arsenal itarudi kwenye ligi baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa, wakiwa na mechi mbili mfululizo za nyumbani, wakiwa na mpango wa kutoka kwenye nafasi ya 11 wanayoshika kwenye msimamo wa ligi kwa sasa. Arsenal itakuwa na kipute cha London derby kwa kuwakabili Crystal Palace na Aston Villa – kabla ya kukipiga na Leeds United nyumbani tena kwenye mechi ya hatua ya 16 bora ya Kombe la Ligi.

Msimu uliopita, Arsenal ilimaliza ligi ikiwa kwenye nafasi ya nane na hivyo kushindwa kufuzu michuano ya Ulaya ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 25 kwa timu hiyo kutocheza michuano ya Ulaya.

Lakini, Carragher anaamini kutokuwapo kwenye michuano ya Ulaya kunawapa faida kubwa Arsenal, kwamba kwa sasa jitihada kubwa zitaelekezwa kwenye michuano ya ligi za ndani.

Kombe la FA na Kombe la Ligi ni michuano mingine inayotoa fursa kwa chama hilo la Arteta kubeba mataji msimu huu ukiweka kando taji la Ligi Kuu England.