Wamiliki wa timu za NBA wanaoongoza kwa mshiko
Muktasari:
- Labda hakuna sehemu inayothibitisha hilo zaidi kama Ligi ya Mpira wa Kikapu Marekani (NBA), ambapo wamiliki wa timu sasa wakijulikana kama magavana wana utajiri wa kutisha wakiishi na kuendesha maisha katika ‘dunia’ yao.
Kundi maarufu la hip hop Wu-Tang Clan liliwahi kuimba “cash rules everything around me.” likimaanisha pesa ndo mtawala wa kila kitu na ni wazi kwamba biti hili linaweza kutumika kuelezea maisha karibu kila sehemu ya dunia.
Labda hakuna sehemu inayothibitisha hilo zaidi kama Ligi ya Mpira wa Kikapu Marekani (NBA), ambapo wamiliki wa timu sasa wakijulikana kama magavana wana utajiri wa kutisha wakiishi na kuendesha maisha katika ‘dunia’ yao.
Hata hivyo, kwa mujibu wa jarida la Forbes, baadhi ya wamiliki wana utajiri unaowatofautisha na wengine. Hawa hapa ni wamiliki 10 tajiri zaidi wa timu za NBA:
1. Steve Ballmer — Dola 121.3 bilioni (Los Angeles Clippers)
Steve Ballmer, aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Microsoft na sasa tajiri mkubwa wa teknolojia, aliinunua Clippers 2014 baada ya Donald Sterling kulazimishwa kuiuza timu hiyo. Ballmer ameijengea Clippers uwanja mpya wa kisasa, Intuit Dome huko Inglewood. Ingawa haijafika fainali za NBA, timu imeimarika.
Ubingwa: Hakuna
Fainali NBA: Hakuna
Fainali Kanda ya Magharibi: 2021
2. Miriam Adelson & Patrick Dumont- Dola 34.6 bilioni (Dallas Mavericks)
Adelson ni mjane wa hayati Sheldon Adelson aliyepata utajiri wake kupitia biashara ya kasino huko Las Vegas. Adelson na mkwe wake Dumont waliinunua Mavericks 2023 kutoka kwa Mark Cuban. Wakiwa na mastaa maarufu na mahiri akiwamo Luka Doncic, Mavericks walifika fainali za NBA 2024.
Ubingwa: Hakuna
Fainali NBA: 2024 Fainali Kanda ya Magharibi: 2024
3. Dan Gilbert - Dola 28.1 bilioni (Cleveland Cavaliers)
Gilbert alipata utajiri wake kupitia kampuni ya mikopo ya nyumba maarufu kama Quicken Loans. Aliinunua Cavaliers 2005, mwaka mmoja baada ya LeBron James kuchaguliwa katika drafti na timu hiyo. Licha ya ugomvi wao wa awali walifanikiwa kushinda ubingwa wa kwanza 2016.
Ubingwa: 2016
Fainali za NBA: 2007, 2015-2018
Fainali Kanda ya Mashariki: 2007, 2009, 2015-2018
4. Stan Kroenke - Dola 16.9 bilioni (Denver Nuggets)
Kroenke ni bilionea wa mali isiyohamishika na mume wa mmoja wa warithi wa familia tajiri anayemiliki utitiri wa maduka ya supamaketi ya Walmart. Alinunua Nuggets mwaka 2000 na kushinda ubingwa wa kwanza 2023. Pia ni mmiliki wa Arsenal na timu ya soka la Kimarekani ya Los Angeles Rams inayoshiriki NFL.
Ubingwa: 2023
Fainali NBA: 2023
Fainali Kanda ya Magharibi: 2009, 2020 na 2023
5. Robert Pera — Dola 13.6 bilioni (Memphis Grizzlies)
Pera ni mwanzilishi na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya vifaa vya mawasiliano ya Ubiquiti Networks. Aliinunua Grizzlies 2012 katika kile kilichoitwa Grit ‘n Grind era. Kwa sasa timu hiyo inamtegemea zaidi Ja Morant kufanikisha mafanikio mapya.
Ubingwa: Hakuna
Fainali NBA: Hakuna
Fainali Kanda ya Magharibi: 2013
6. Antony Ressler - Dola 11.6 bilioni (Atlanta Hawks)
Ressler alipata utajiri kupitia kampuni za uwekezaji za Apollo Global Management na Ares Management. Aliinunua Hawks 2015. Timu hiyo imekuwa ya kawaida katika ligi hiyo na mafanikio makubwa iliyoyapata tangu ianzishwe ni kufika Fainali Kanda ya Magharibi 2021.
Ubingwa: Hakuna
Fainali NBA: Hakuna
Fainali Kanda ya Mashariki: 2021
7. Tilman Fertitta - Dola 10.2 bilioni (Houston Rockets)
Fertitta alipata utajiri kupitia sekta za chakula, burudani na kasino. Anamiliki Fertitta Entertainment. Aliinunua Rockets 2017, na chini ya supastaa wa kikapu James Harden ilifanya vizuri msimu wa kawaida, lakini haikuvuka Fainali Kanda ya Magharibi 2018.
Ubingwa: Hakuna
Fainali NBA: Hakuna
Fainali Kanda ya Magharibi: 2018
8. Tom Gores — Dola 9.4 bilioni (Detroit Pistons)
Gores ni bilionea wa uwekezaji binafsi akiendesha kampuni ya Platinum Equity. Aliinunua Pistons 2011 na kuwa mmiliki mkuu 2015. Mafanikio yake makubwa ni kuhamisha timu kurudi katikati ya Jiji la Detroit.
Ubingwa: Hakuna
Fainali NBA: Hakuna
Fainali Kanda ya Mashariki: Hakuna
9. Joseph Tsai — Dola 9.3 bilioni (Brooklyn Nets)
Tsai ni mwanzilishi mwenza wa kampuni ya Alibaba Group, ambapo aliinunua Nets 2019, lakini bado hajafanikiwa kuifikisha popote. Mradi wa mastaa Kevin Durant, Kyrie Irving na James Harden ulishindikana kuifanya ing’are. Kwa sasa ina mpango mpya wa kujenga timu.
Ubingwa: Hakuna
Fainali NBA: Hakuna
Fainali Kanda ya Mashariki: Hakuna
10. Micky Arison - Dola 8.8 bilioni (Miami Heat)
Arison ni mwenyekiti wa Carnival Corporation, kampuni kubwa ya meli za utalii duniani. Aliirithi timu hiyo kutoka kwa baba yake 1995 na ameiongoza kuwa na mafanikio ya makubwa. Chini yake, Miami Heat imeshinda ubingwa mara tatu na kufika fainali mara nyingi.
Ubingwa: 2006, 2012, 2013
Fainali za NBA: 2006, 2011, 2012, 2014, 2020 na 2023
Fainali Kanda ya Mashariki: 1997, 2005, 2006, 2011, 2013, 2014, 2020, 2022 na 2023