Denver Nuggets ya Jokic inavyoanza upya NBA
Muktasari:
- Akiingia msimu wake wa 11 tangu ajiunge na Nuggets 2015, Jokic amesema mkataba mkubwa unaosubiriwa msimu ujao siyo kipaumbele kwake, bali ni malipo ya juhudi za muda mrefu kwenye mchezo huo.
DENVER, MAREKANI: DENVER Nuggets imeingia msimu mpya wa NBA 2025/26 ikiwa na ari mpya na mabadiliko ya kikosi, huku Nikola Jokic akieleza dhamira yake ya kubaki na klabu hiyo.
Akiingia msimu wake wa 11 tangu ajiunge na Nuggets 2015, Jokic amesema mkataba mkubwa unaosubiriwa msimu ujao siyo kipaumbele kwake, bali ni malipo ya juhudi za muda mrefu kwenye mchezo huo.
Jokic anayejulikana kwa jina la utani 'The Joker' alikataa kusaini ofa ya mkataba wa miaka minne wenye thamani ya Dola 212 milioni msimu huu akijua ujao anaweza kusaini mkataba wa thamani ya Dola 293 milioni.
Kwa sasa anabaki na mkataba wa 'supermax' wa miaka mitano wenye thamani ya Dola 276 milioni aliouingia 2022.
“Kwangu mikataba hii ni kama zawadi. Kitu cha kawaida kwenye mchezo hasa katika NBA ya leo ambapo kiwango cha mishahara kinaongezeka kila mwaka,” anasema Jokić. “Lakini mpango wangu ni kuwa Nugget daima.”
MABADILIKO NUGGETS
Baada ya kutwaa taji la kwanza la NBA 2023, Nuggets walipitia mabadiliko makubwa kwenye uongozi na kikosi, ambapo uongozi uliondoa kibarua cha muda cha kocha David Adelman na kumpa mamlaka kamili wakati nafasi ya meneja mkuu ilichukuliwa na Ben Tenzer na Jonathan Wallace baada ya Calvin Booth kuondoka.
Katika kikosi, Nuggets ilifanya biashara kubwa kwa kumtoa Michael Porter Jr kwenda Brooklyn Nets na kumchukua mtupiaji mahiri Cam Johnson. Hatua hiyo pia ilitoa nafasi ya kupunguza matumizi ya mishahara na kuongeza upana wa kikosi. Vilevile imemuingiza nyota wa zamani Bruce Brown aliyekuwa sehemu muhimu ya ubingwa wa 2023 pamoja na Tim Hardaway Jr na Jonas Valanciunas ambaye atakuwa msaidizi muhimu wa Jokic.
Nuggets inatarajia kumrejesha DaRon Holmes kwenye kiwango chake akiwa ni chaguo la drafti 2024 ambaye alikosa msimu wake wa kwanza kutokana na jeraha. “Tumepata wachezaji wapya wengi Bruce amerudi. Tulishinda naye. Tuna Cam, Jonas, Holmes akiwa mzima kiafya. Kuna nguvu mpya, mwanzo mpya. Tunatarajia kufanya kitu kikubwa,” anasema Jokic.
KURUDI KWA BRUCE BROWN
Bruce Brown aliyesaidia Nuggets kushinda ubingwa wa kwanza, lakini akajiunga na Indiana Pacers kwa mkataba mnono anasema alitamani kurejea mapema zaidi. Baada ya kutimkia Toronto Raptors kwa muda mfupi Brown anasema alikuwa akihisi Nuggets ndiko nyumbani kwake.
“Toronto walikuwa kwenye hatua ya kujijenga upya nami nilihisi niko sehemu tofauti ya maisha yangu ya kitaaluma. Niliwaza mapema tu kwamba ningependa kurudi Denver,” anasema Brown.
CHANGAMOTO MPYA
Licha ya ushindani mkali kutoka timu kama Oklahoma City Thunder waliowang'oa Nuggets katika mchezo wa saba wa hatua ya nusu fainali ya Ukanda wa Magharibi kabla ya kutwaa ubingwa wa NBA msimu uliopita, Nuggets wanaamini kuwa maboresho yatawapa nafasi nzuri ya kurejea kileleni.
Kihistoria, Nuggets hawajawahi kufika fainali zaidi ya mara moja, lakini sasa wanaanza kuonekana kama moja ya vikosi vilivyo tishio Magharibi. Kurejea kwa Jokic akiwa na ari mpya pamoja na uongozi ulioimarishwa na wachezaji wazoefu, mashabiki wao wana matumaini kuwa msimu wa 2025/26 unaweza kuwa wa kihistoria.
Msimu wa NBA ukianza Oktoba macho ya wengi yatakuwa kwa The Joker na Nuggets kufuatili kama wanaweza kurudia mafanikio ya 2023 au hata kuvuka. Jokic aliyeshinda mara tatu tuzo ya MVP wa NBA (2021, 2022 na 2023) ana nafasi ya kuandika historia zaidi ikiwa ataendelea kuwa na Nuggets.
Kwa sasa, anasema jambo muhimu siyo mkataba au fedha, bali ni kufanya makubwa akiwa na timu hiyo. “Natamani mashabiki wanaponiangalia siku moja wakumbuke siyo tu namba nilizoweka, bali roho niliyoleta kwenye mchezo na kwenye Denver Nuggets,” anasema Jokic.