Wakala wa Haaland afichua siri ya mkataba mpya
Muktasari:
- Straika huyo wa Norway ameonekana kuwa usajili wenye mafanikio makubwa tangu alipowasili kutoka Borussia Dortmund mwaka 2022 na tangu wakati huo, amefunga mabao 160 katika mechi 195 za mashindano yote.
MANCHESTER, ENGLAND: WAKALA wa Erling Haaland amesema hawakuwa na nguvu yoyote ya kushinikiza kupata masilahi makubwa zaidi kwa Manchester City wakati wa mazungumzo ya kuongeza mkataba wa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Norway.
Straika huyo wa Norway ameonekana kuwa usajili wenye mafanikio makubwa tangu alipowasili kutoka Borussia Dortmund mwaka 2022 na tangu wakati huo, amefunga mabao 160 katika mechi 195 za mashindano yote.
Mchezaji huyo, 25 amekuwa akihusishwa na uwezekano wa kuondoka huku Real Madrid ikitajwa ni miongoni mwa timu zinazomtaka.
Hata hivyo, msimu uliopita Haaland alisaini mkataba mpya na Man City ambao utamweka katika viunga vya Etihad hadi mwaka 2034.
Akitoa maelezo kuhusu mazungumzo ya mkataba huo, wakala wake Rafaela Pimenta amesema Man City ndio walikuwa na udhibiti mkubwa katika mazungumzo hayo tangu mwanzo.
Akizungumza na ESPN, Pimenta amesema: "Wako makini sana, wamejipanga vizuri sana. Ni klabu kubwa mno. Wanajua wanachofanya, wana uzoefu mkubwa, hawahitaji chochote kwa sababu tayari wana kila kitu. Hivyo sisi hatukuwa na nguvu yoyote ya kuwabana.”
Pimenta pia alimzungumzia Haaland mwenyewe akisema kwa wakati huo akili yake ilikuwa inamtuma tu aendelee kusalia Man City akiamini ataendeleza kiwango chake zaidi akiwa katika viunga hivyo badala ya kuondoka.