Waachana baada ya uchumba wa siku tatu
Muktasari:
- Derrickson Quiros alisambaa mitandaoni baada ya kupiga goti moja na kumposa mpenzi wake kwenye Uwanja wa Estadio Mario Camposeco.
GUATEMALA CITY, GUATEMALA: STAA mmoja wa soka ametangaza kuwa ameachana na mchumba wake siku tatu tu baada ya kumvisha pete ya uchumba uwanjani.
Derrickson Quiros alisambaa mitandaoni baada ya kupiga goti moja na kumposa mpenzi wake kwenye Uwanja wa Estadio Mario Camposeco.
Quiros alitoa posa hiyo baada ya Club Xelaju kushinda mabao 4-2 dhidi ya Deportivo Marquense katika ligi kuu ya Guatemala.
Mamia ya mashabiki waliwashangilia wawili hao na kuwapongeza kwa makofi kufuatia uchumba wao.
Kiungo huyo alishiriki tukio hilo la kugusa moyo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, akiandika: “Mwenza wa maisha yangu, nakupenda sana.”
Hata hivyo, siku tatu tu baadaye, alitangaza kuwa wameachana katika taarifa iliyowashangaza wengi.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, ambako ana wafuasi takriban 10,000, alinukuliwa na tovuti ya Mexico ya Latinus akisema: “Ndiyo, ni kweli kwamba uhusiano wangu umefikia mwisho.
“Ilikuwa hali ngumu binafsi, kama ilivyo kwa kila kuachana, lakini napendelea kushughulikia suala hili kwa heshima na ukomavu.
“Sitamsema vibaya mtu yeyote, wala sitaingia kwa undani, kwa sababu ulikuwa uhusiano muhimu kwangu kwa wakati wake.”
Mchumba wake wa zamani naye alivunja ukimya kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii.
Kama ilivyoripotiwa na Globo, aliandika: “Mwisho wa siku, hakutakuwa na jibu bora zaidi kuliko lile linalotolewa na ukimya.”
Mchezaji huyo wa Costa Rica aliongeza: “Kwa sasa nimejikita kwenye taaluma yangu, timu yangu, na kuendelea kukua kama mtu.”
“Nashukuru kwa msaada wa kila mmoja na natumaini wataheshimu kipindi hiki. Asanteni.”