Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vita ya ‘top 4’ England yapamba moto, Man United chali

Muktasari:

  • Zikiwa zimesalia mechi chache kumalizika kwa msimu huu bado mbio za kuwania nafasi nne za juu katika Ligi Kuu England zinaendelea.

LONDON, ENGLAND: Vita ya kuwania nafasi nne za juu katika Ligi Kuu England (EPL) msimu huu imechukua sura mpya baada ya mechi za jana Jumapili, Mei 4, 2025 kuchezwa, huku Chelsea ikipata ushindi dhidi ya mabingwa wapya Liverpool na kuisogelea Newcastle iliyolazimishwa sare na Brighton.

Chelsea ilionyesha ubora wa hali ya juu katika Uwanja wa Stamford Bridge kwa kuifunga Liverpool mabao 3-1, ushindi ambao umeiweka katika nafasi ya tano ikiwa na pointi 63, sawa na Newcastle huku zikitenganishwa na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Bao la mapema la Enzo Fernández, bao la kujifunga la Jarell Quansah na penalti ya dakika za nyongeza iliyopigwa na Cole Palmer ilitosha kuipa Chelsea ushindi huo pamoja na pointi tatu muhimu, huku bao pekee la Liverpool likifungwa na beki, Virgil van Dijk katika dakika ya 85.

Katika mechi nyingine , ilishuhudiwa Newcastle wakinusurika kufungwa na Brighton baada ya Alexander Isak kusawazisha kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 89 na kulazimisha sare ya bao 1-1. Newcastle sasa wapo katika nafasi ya nne wakiwa na pointi 65 huku Brighton ikishika nafasi ya 10 ikiwa na pointi 52.

Manchester United iliendelea kugubikwa na wimbi la matokeo mabaya baada ya kuchapwa mabao 4-3 na Brentford katika mechi iliochezwa ugenini kwenye Uwanja wa Gtech Community. Hii ilikuwa ni mechi ya 16 kwa United kupoteza msimu huu ikiwa ni rekodi mbaya zaidi katika historia ya EPL.

Bao la mapema la Mason Mount katika dakika ya 14 liliwaweka wageni hao mbele, lakini Brentford walisawazisha haraka kupitia bao la kujifunga la Luke Shaw katika dakika ya 27.

Dakika sita baadaye, Kevin Schade ambaye alifunga mabao mawili aliipa Brentford bao la uongozi akiunganisha kwa kichwa mpira wa krosi iliyochongwa nahodha Christian Nørgaard kabla ya kurejea tena kufunga katika dakika ya 70 na kuongeza bao la tatu akiunganisha kwa kichwa krosi ya Bryan Mbeumo.

Yoane Wissa aliifungia Brentford bao la nne katika dakika ya 74, akimalizia pasi ya Mikkel Damsgaard, na kufanya mambo kuwa magumu kwa vijana wa Ruben Amorim.

Manchester United inashika nafasi ya 15 ikiwa na pointi 39 katika michezo 35 iliyocheza wakati Brentford ikiwa inashika nafasi ya tisa kwa pointi 52 ilizokusanya hadi sasa.

Hata hivyo, United walijaribu kurejea mchezoni kupitia mabao mawili ya haraka yaliyofungwa na Alejandro Garnacho katika dakika ya 82 akipiga shuti kali nje ya boksi wakati Amad Diallo akifunga lingine katika dakika za majeruhi , lakini mabao hayo hayakuweza kuiokoa United.

Katika mchezo mwingine, ilishuhudiwa wenyeji wa mchezo West Ham wakitoshana nguvu na Tottenham baada ya kumaliza mchezo kwa sare ya bao 1-1, matokeo ambayo yamewaacha Spurs wakijikokota katika nafasi ya 16 wakiwa na pointi 38 mbele ya West Ham ambao wanashika nafasi ya 17 wakiwa na pointi 37.