Virgil van Dijk amvaa staa wa Everton
Muktasari:
- James Tarkowski alifunga bao la kusawazisha dakika ya 98 kwa Everton na Van Dijk anadhani Doucoure alichochea mivutano baada ya mechi na watu wanne walionyeshwa kadi nyekundu ikiwemo Arne Slot, msaidizi wake Sipke Hulshoff, Curtis Jones na Doucoure.
LIVERPOOL, ENGLAND: NAHODHA wa Liverpool, Virgil van Dijk, amemuonya kiungo wa Everton, Abdoulaye Doucoure, kwa kuanzisha ugomvi uwanjani wakati wa mchezo wao wa Ligi Kuu England, usiku wa jana Jumatano.
James Tarkowski alifunga bao la kusawazisha dakika ya 98 kwa Everton na Van Dijk anadhani Doucoure alichochea mivutano baada ya mechi na watu wanne walionyeshwa kadi nyekundu ikiwemo Arne Slot, msaidizi wake Sipke Hulshoff, Curtis Jones na Doucoure.
Kiungo huyo alianzisha vurugu hizo kwenye jukwaa la mashabiki wa Liverpool hali iliyochochea ugomvi katika dabi hiyo ya Merseyside.
“Mlioona walivyosherehekea goli, wana haki yao yote kufanya hivyo. Doucoure alienda kuchokoza mashabiki wetu. Curtis alienda kugombana naye kwa sababu aliona hakikuwa kitu cha busara kufanya. Mwamuzi hakuwa na udhibiti wa mchezo. Nilimwambia hivyo,” alisema Van Dijk.
“Ilikuwa uchochezi mkubwa kutoka kwa mchezaji mmoja. Sote tuliona na tukajaribu kupambana na hilo kadri tulivyoweza. Unajua chochote kinachotokea kiwanjani anayepaswa kushughulika nacho ni mwamuzi na leo (juzi) sidhani kama alikishughulikia hilo kikamilifu.”
Baadhi ya mashabiki walivamia uwanja wakati wa vurugu hizo.
Beto aliwafungia Everton bao la kuongoza dakika ya 11 lakini Alexis Mac Allister alisawazisha haraka kisha Mohamed Salah akafunga la pili dakika ya 73 kabla ya Everton kusawazisha.
Akizungumzia hali ya mgogoro ulioibuka dakika za mwisho za mchezo huo, kocha wa Everton David Moyes alisema: “Sikuliona tukio vizuri kutokana na mahali nilipokuwa.”
Kutokana na kadi nyekundu, Slot na msaidizi wake namba mbili hawakuruhusiwa kufanya mahojiano na vyombo vya habari na wakati wa mchezo kocha msaidizi namba mbili Johnny Heitinga ndio atakayesimama kwenye benchi.