Vinicius, Real Madrid mambo yamenoga
Muktasari:
- Mkataba wa sasa wa Vinicius unatarajiwa kumalizika mwaka 2027 na awali ilionekana huenda asiongezewe kwa sababu hana furaha juu ya namna kocha wa timu hiyo, Xabi Alonso anavyomchezesha na mara kadhaa amekuwa akifanyiwa mabadiliko na hata kutochezeshwa.
MADRID, HISPANIA: TAARIFA za ndani zinaeleza wawakilishi wa Real Madrid na wale wa Vinicius Junior wamefikia makubaliano kamili ya kumuongeza mkataba mpya Mbrazil huyo kwa muda mrefu zaidi.
Mkataba wa sasa wa Vinicius unatarajiwa kumalizika mwaka 2027 na awali ilionekana huenda asiongezewe kwa sababu hana furaha juu ya namna kocha wa timu hiyo, Xabi Alonso anavyomchezesha na mara kadhaa amekuwa akifanyiwa mabadiliko na hata kutochezeshwa.
Taarifa kutoka tovuti ya AS zimefichua staa huyo, 25, ameamua kusaini mkataba huo mpya bila ya kujali kile kinachoendelea kati yake na kocha.
Mazungumzo ya mkataba huo mpya yanadaiwa yalianza Mei na yalisimama kwa vipindi kadhaa kabla ya kurejea mapema mwezi huu na ndiyo wamefikia mwakafa.
Vinicius kwa sasa anapata mshahara wa Euro 400,577 kwa wiki lakini katika mkataba huo mpya anaweza kulipwa Euro 600,000 kwa wiki mbali ya bonasi.
Suala la Vinicius kufikia makubaliano ya kusaini mkataba mpya linalonekana kuwashangaza wengi kutokana na kile kilichotokea siku kadhaa nyuma na alitamka hadharani bora aondoke kuliko kuendelea kucheza Madrid baada ya kufanyiwa mabadiliko katika mechi ya El Classico.
Kauli hizo ziliibua tetesi anaweza akatimkia PSG au Saudi Arabia ambako Al-Hilal ipo tayari kumpa ofa nono sana.