Vinicius akutana na matajiri wa Saudia
Muktasari:
- Mchezaji huyu raia wa Brazil amekuwa muhimu katika mafanikio ya Real Madrid kwenye miaka ya hivi karibuni na ameanza kuhusishwa na matajiri hao tangu mwaka jana.
MADRID, HISPANIA: STAA wa Real Madrid, Vinicius Junior anaripotiwa kukutana na maafisa kutoka Ligi Kuu ya Saudi Arabia wanaojaribu kutaka kumsajili dirisha lijalo.
Mchezaji huyu raia wa Brazil amekuwa muhimu katika mafanikio ya Real Madrid kwenye miaka ya hivi karibuni na ameanza kuhusishwa na matajiri hao tangu mwaka jana.
Hata hivyo, ripoti kutoka Hispania zimedai kuna uwezekano mkubwa Vinicius akaondoka mwisho wa msimu huu kutokana na ofa kubwa iliyowekwa na matajiri hao wa Saudia.
Kwa mujibu wa tovuti ya Marca, maafisa kutoka Saudi Arabia walikutana na Vinicius kwa mara ya kwanza mwaka juzi huko Prague, Jamhuri ya Czech ambaye walifanya naye mazungumzo ya kumsajili kwa wakati huo na ikashindikana.
Inaripotiwa baada ya hapo, staa huyu amekuwa akizungumza na makamu rais wa ligi hiyo, Saad Al Lazeez ambaye ndiyo ameweka urafiki naye wa karibu.
Matajiri hao ambao wanafanya kazi chini ya mfumo wa Saudi Investment Fund inayomiliki zaidi ya timu tatu za ligi hiyo, wapo tayari kumpa Vinicius mkataba wa miaka mitano utakaokuwa na thamani ya Pauni 830 milioni.
Mkataba huo pia inaripotiwa utamfanya mchezaji huyo kuwa balozi wa Kombe la Dunia la 2034 litakalofanyika nchini humo.
Wanachama wa msafara wake wanaripotiwa kuona pendekezo lililotolewa kama kubwa na ngumu kukataa kutokana wingi wa pesa. Alipoulizwa baada ya mechi dhidi ya Man City kuhusu uvumi unaozunguka juu ya mustakabali wake, Vinicius alisisitiza anataka kuendelea na urithi wake katika mji huo mkuu wa Hispania kwa miaka ijayo.
“Sijui chochote pia. Sijazungumza na mtu yeyote bado. “Naona inabidi nizungumze na rais. Natumai naweza kubaki hapa kwa muda mrefu. Hapa ndiko nyumbani kwangu,”alisema Vinicius.