Vini Jr agomea mkataba Madrid
Muktasari:
- Vinicius, 24, mkataba wake wa sasa huko Los Blancos unamshuhudia akilipwa Pauni 12.5 milioni kwa mwaka na dili hilo litafika ukomo 2027 huku kwenye kandarasi hiyo kukiwekwa kipengele kinachotaja kiasi kinachofaa kuvunja dili hilo, Pauni 830 milioni kama kutakuwa na timu nyingine inamtaka.
MADRID, HISPANIA: LISEMWALO ni Vinicius Junior amegomea mkataba mpya Real Madrid jambo linalozidi kuchochea uvumi wake wa kutimkia Saudi Arabia, imeelezwa.
Vinicius, 24, mkataba wake wa sasa huko Los Blancos unamshuhudia akilipwa Pauni 12.5 milioni kwa mwaka na dili hilo litafika ukomo 2027 huku kwenye kandarasi hiyo kukiwekwa kipengele kinachotaja kiasi kinachofaa kuvunja dili hilo, Pauni 830 milioni kama kutakuwa na timu nyingine inamtaka.
Staa huyo wa Kibrazili ameripotiwa kuwawindwa na klabu za Saudi Arabia na zipo tayari kuvunja benki kwa ajili yake ili akacheze Mashariki ya Kati.
Kikao kimefanyika baina ya mawakala wa Vini na mabosi wa klabu za Saudia, Desemba mwaka jana kwa ajili ya kumnasa staa huyo, huku ikielezwa mchakato huo ulianza tangu kwenye dirisha la uhamisho la majira ya kiangazi la mwaka jana.
Kuona hivyo, mabosi wa Los Blancos waliamua kuwaita mawakala wa Vini mezani ili wamsainishe dili refu ambalo litawakala kilimikilimi matajiri wa Saudi Pro League. Kinachoelezwa ni ofa ya Real Madrid imegomewa kwa sababu haina ushawishi, lakini mazungumzo bado yanaendelea.
Mabosi wa Saudia wanaraka kumpa Vini mshahara wa Pauni 168 milioni kwa mwaka kwenye dili lao la zaidi ya miaka mitano, ambalo litakuwa na thamani ya Pauni 865 milioni.
Hata hivyo, Real Madrid haina mpango wa kumuuza Vini, hivyo kama kutakuwa na timu inataka saini yake, basi italazimika kulipa pesa nyingine, pengine ile inayokaribia kipengele kilichowekwa kwenye mkataba wake ili waruhusu Mbrazili huyo aondoke Bernabeu.
MAVITU WA VINI REAL MADRID MSIMU WA 2024-25
-Amecheza: Mechi 16
-Ametengeneza: Nafasi 31
-Amefunga: Mabao 8
-Ametoa: Asisti 5
-Amelenga golini: Mashuti 14
-Amepiga: Pasi 447