Vigogo watano wote macho kwa Mbappe

Muktasari:

ISHAKUWA soo. Kocha wa Paris Saint-Germain, Mauricio Pochettino amekiri kwamba hana uhakika kama Kylian Mbappe atabaki kwenye timu hiyo wakishindwa kunyakua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

LIVERPOOL, ENGLAND. ISHAKUWA soo. Kocha wa Paris Saint-Germain, Mauricio Pochettino amekiri kwamba hana uhakika kama Kylian Mbappe atabaki kwenye timu hiyo wakishindwa kunyakua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

PSG ipo kwenye hatari ya kutupwa nje kwenye michuano hiyo baada ya kuchapwa 2-1 nyumbani na Manchester City katika mchezo wa kwanza wa hatua ya nusu fainali ya mikikimikiki hiyo.

Mkataba wa Mbappe utafika tamati 2022 na alipoulizwa kuhusu hatima ya mshambuliaji huyo, Pochettino alitoa maelezo kwamba PSG, “tunafanya kila kitu kuhakikisha anabaki”.

Kisha alisema: “Hilo ni swali linalomhusu Kylian na sio mimi. Tumepoteza mechi lakini bado kuna mechi ya marudiano na mambo ya ajabu yamekuwa yakitokea kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Yeye ana mwaka mmoja bado kwenye mkataba wake.

“Nilishasema huko nyuma, lakini klabu na mimi tunafanya kwa kila tunaloweza kuhakikisha anabaki kwa miaka mingi. Klabu inafanyika kazi jambo hilo na Kylian Mbappe anafuraha kuwa nasi. Tuna mwezi mmoja umebaki kwenye michuano ili kufikia matarajio yetu na bado tupo kwenye mbio.” Na kama Mbappe ataamua kuondoka, wapi ataweza kwenda? Kuna orodha ya klabu tano ambazo Mbappe anaweza kwenda kuanza maisha mapya na kujitengenezea himaya kubwa kama ataamua kuachana na PSG kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Liverpool ni klabu ya kwanza ambayo imekuwa ikihusishwa kunasa huduma ya Mbappe na kocha Jurgen Klopp ni shabiki mkubwa wa mchezaji huyo, huku nyuma aliwahi kuiambia RMC Sport: “Nampenda, kwa kusema ukweli. Ni mchezaji wa aina yake na hakika ni kijana mzuri. Ni bonge la mchezaji, bonge la mchezaji.”

Mbappe naye amekuwa akizungumzia vizuri Liverpool chini ya Klopp, akisema: “Kile wanachokifanya Liverpool ni balaa. Wamekuwa kama mashine.”

Timu ya pili ni Real Madrid. Miamba hiyo ya La Liga imekuwa uhusishwa sana na Mbappe na kwa mujibu wa gazeti la Hispania la Sport, tatizo la kiuchumi linalowakabili Los Blancos haliwezi kuwazuia kumsajili Mbappe kwa namna wanavyohitaji saini yake. Limedai kwamba Real Madrid wapo tayari kumtoa beki Raphael Varane na mshambuliaji Vinicius Junior kwenda PSG kama ofa ya kumchukua Mbappe ili kushusha bei anayouzwa.

Mbappe mwenyewe huko nyuma aliwahi kusema kocha wa sasa wa Real Madrid, Zinedine Zidane ndiye aliyekuwa shujaa wake wa kwanza na anaona kuna uwezekano wa kwenda kufanya naye kazi Bernabeu.

Timu ya tatu kwenye rada za Mbappe ni Man City. Miamba hiyo ya Etihad inayonolewa na Pep Guardiola itakwenda kuachana na straika wake Sergio Aguero mwishoni mwa msimu huu mkataba wake utakapokwisha, hivyo wataingia sokoni kunasa mshambuliaji mpya na Mbappe wanamwona ni mtu anayeweza kufiti kwenye buti hizo.

Kwa mujibu wa gazeti la Ufaransa, Le Parisien, Man City ni miongoni mwa klabu zinazovutiwa na mpango wa kumsajili Mbappe, hivyo wapo tayari kuvunja benki kukamilisha jambo hilo.

Timu ya nne ni Juventus. Miamba hiyo ya Italia, inafahamu wazi supastaa wao Cristiano Ronaldo amekuwa akihusishwa na mpango wa kuondoka mwishoni mwa msimu huu na kama hilo litatokea, basi Juventus itakuwa na pesa za kutosha kwenda kunasa huduma ya Mbappe.

Kwa mujibu wa gazeti la L’Equipe, Ronaldo analipwa Pauni 900,000 kwa wiki huko Juventus na kama ataondoka, basi mshahara huo unatosha kabisa kumlipa Mbappe na akashawishika.