Victor Wembanyama alazimisha mechi saba NBA
Muktasari:
- Baada ya kupoteza vibaya mchezo 5, Spurs walijibu kwa kishindo katika mchezo wa 6 kwa kuichapa Thunder kwa pointi 118-91 mbele ya mashabiki wao na kusawazisha mfululizo huo kuwa 3-3.
LOS ANGELES, MAREKANI: NYOTA wa San Antonio Spurs, Victor Wembanyama, amesema ari ya kupambana kama timu iliyokuwa ukingoni mwa kutolewa ndiyo siri ya ushindi mkubwa walioupata dhidi ya Oklahoma City Thunder na kulazimisha mchezo wa saba wa fainali za Ukanda wa Magharibi.
Baada ya kupoteza vibaya mchezo 5, Spurs walijibu kwa kishindo katika mchezo wa 6 kwa kuichapa Thunder kwa pointi 118-91 mbele ya mashabiki wao na kusawazisha mfululizo huo kuwa 3-3.
Wembanyama alikuwa gumzo kubwa katika mchezo huo baada ya kufunga pointi 28 ndani ya dakika 29 pekee, huku akiongeza rebounds 10 na blocks tatu.
Katika mchezo wa 5, nyota huyo wa ulinzi alikuwa sehemu ya kikosi kilichoshindwa kuhimili nguvu ya Thunder, lakini safari hii alionyesha tofauti kubwa.
Kocha wa Spurs, Mitch Johnson, amesema kilichobadilika kwa Wembanyama ni kiwango chake cha kujituma na dhamira ya kuacha alama ndani ya mchezo.
“Shughuli yake uwanjani ilikuwa kubwa zaidi. Alikuwa na nia ya kweli ya kuutawala mchezo,” amesema Johnson.
Baada ya ushindi huo, Wembanyama amesema Spurs walicheza kwa utulivu na kuamini mfumo wao wa mchezo.
“Tulikuwa thabiti na tukafanya kile tulichopaswa kufanya. Tuliamini mchezo huu utamalizika kwa faida kwetu,” amesema nyota huyo mwenye umri wa miaka 22.
Mbali na kiwango chake binafsi, Wembanyama aliwasifu wachezaji wa benchi wa Spurs waliochangia pointi 46 muhimu katika ushindi huo.
Spurs walitawala mchezo tangu mwanzo huku Wembanyama akifunga pointi 11 katika robo ya kwanza, akitumia vyema mitupo ya mbali. Katika safu ya ulinzi, Spurs waliizuia Thunder kufunga kwa asilimia 37.2 pekee za mashuti yao yote na asilimia 25 kutoka nje ya mstari wa pointi tatu.
Johnson amesema licha ya Wembanyama kutokuwa mkamilifu wakati wote, anaonesha kukua kiakili na kubeba majukumu makubwa ya timu.
“Ni kijana wa miaka 22 tu lakini ana ujasiri mkubwa wa kubeba presha na majukumu ya timu.” amesema kocha huyo.
Baada ya kipigo cha mchezo wa 5, Wembanyama alionekana mwenye hasira kubwa. Kamera za NBC zilimuonesha akizungumza na Mason Plumlee muda mfupi kabla Plumlee hajamfanyia madhambi makali Jared McCain.
Katika mchezo wa 6, Spurs waliongeza ugumu wa mchezo. Wembanyama alimwangusha Cason Wallace katika robo ya pili huku Carter Bryant naye akimvaa kwa nguvu Shai Gilgeous-Alexander.
Spurs walitawala pia kwenye rebounds kwa 52 dhidi ya 42 na kufunga pointi nyingi zaidi ndani ya eneo la chini ya kikapu, 44 kwa 38. Nyota wa Thunder, Shai Gilgeous-Alexander, alikiri wazi kuwa Spurs walikuwa bora zaidi kimwili.
Macho yote yataelekezwa katika mchezo wa 7 utakaopigwa leo huku Thunder wakiwa na faida ya kucheza nyumbani.