Vicario aiokoa Spurs kwa Monaco
Muktasari:
- Vicario, raia wa Italia ambaye amekuwa akikosolewa msimu huu, ndiye sababu kubwa iliyowafanya Spurs kuondoka Stade Louis II na sare licha ya kucheza chini ya kiwango.
Kipa wa Tottenham Hotspur, Guglielmo Vicario, usiku wa Oktoba 22, 2025 alifanya kazi kubwa kwa kuizuia Monaco, huku kikosi cha Thomas Frank kikinusurika na kupata pointi moja ya Ligi ya Mabingwa.
Vicario, raia wa Italia ambaye amekuwa akikosolewa msimu huu, ndiye sababu kubwa iliyowafanya Spurs kuondoka Stade Louis II na sare licha ya kucheza chini ya kiwango.
Katika kipindi cha kwanza, aliokoa mikwaju minne ya hatari, mitatu kati yake dhidi ya mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Folarin Balogun, na mwingine dhidi ya Maghnes Akliouche.
Spurs ililazimika kujilinda kwa nguvu dhidi ya Monaco ambayo hivi karibuni ilitoka sare ya 2-2 na Manchester City, lakini nayo ilikaribia kufunga kupitia kichwa cha Micky van de Ven kilichopaa juu ya lango kabla ya mapumziko.
Kipindi cha pili kiligeuka kuwa kama onyesho la Vicario, baada ya kipa huyo tena kuzuia juhudi za Akliouche na Balogun, kabla ya kuonyesha ubora zaidi kwa kuokoa kwa ustadi mpira wa kichwa wa Jordan Teze aliyekuwa karibu kabisa.
Kiungo wa zamani wa Liverpool, Takumi Minamino, pia alikosa nafasi tatu nzuri, jambo lililomfanya kocha Frank kushukuru angalau kupata pointi moja ugenini kutokana na ukuta imara ulioongozwa na Vicario.