VAR ilivyoibeba Man United bao la jioooni
Muktasari:
- Beki wa zamani wa Leicester City, Harry Maguire alifunga kwa kichwa bao la ushindi kwa Man United dakika za mwisho na kuifanya miamba hiyo ya Old Trafford kushinda 2-1 na kutinga raundi ya tano ya michuano hiyo.
MANCHESTER, ENGLAND: RUUD van Nistelrooy amefyumu baada ya kikosi chake cha Leicester City kutupwa nje ya Kombe la FA kwa bao la utata kwenye dakika za majeruhi dhidi ya Manchester United uwanjani Old Trafford juzi Ijumaa usiku.
Beki wa zamani wa Leicester City, Harry Maguire alifunga kwa kichwa bao la ushindi kwa Man United dakika za mwisho na kuifanya miamba hiyo ya Old Trafford kushinda 2-1 na kutinga raundi ya tano ya michuano hiyo.
Maguire kabla ya kufunga bao hilo alionekana kabisa yupo kwenye nafasi ya kuotea. Teknolojia ya video inayomsaidia mwamuzi (VAR) haitumiki kwenye raundi ya tatu ya michuano hiyo na hilo ndilo lililoifanya Man United kushinda mchezo huo kwa bao la kuotea ambalo halikuonekana na waamuzi wa uwanjani na itaanza kutumika kwenye raundi ya tano ya Kombe la FA.
Kocha wa muda wa zamani wa Man United, ambaye kwa sasa ndiye anayeinoa Leicester City, Van Nistelrooy alikasirishwa na kusema VAR ilipaswa kutumika hata kweye raundi hiyo ya Kombe la FA.
Alisema: "Hakufungwa kwenye ile Fergie time, tumefungwa na offside time. Ile haikuwa na ulazima wa kuwapo na VAR. Kwa sababu VAR inaamua kuotea kwa sentimeta chache au inchi chache, lakini ile ilikuwa karibu nusu mita. Ile ilikuwa ngumu sana kuielewa kwa sababu timu yangu ilistahili sare. Kisha mechi iingie kwenye dakika za nyongeza, huwezi kujua nini kingetokea."
Katika mchezo huo, Leicester City ilitangulia kwa bao lililofungwa na Bobby Decordova-Reid kwenye kipindi cha kwanza, lakini Man United ilisawazisha kupitia kwa straika mtokea benchini, Joshua Zirkzee kabla ya Maguire kufunga la ushindi kwenye dakika za majeruhi.