Van Persie kupewa mikoba Feyenoord
Muktasari:
- Mdachi huyo alianza kazi yake ya ukocha kwenye klabu ya Rotterdam na sasa atarejea mzigoni baada ya kukubali kwenda kuinoa Feyenoord, timu ambayo imetinga hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
AMSTERDAM, UHOLANZI: ROBIN van Persie amefikia makubaliano ya kuwa kocha mpya wa Feyenoord.
Mdachi huyo alianza kazi yake ya ukocha kwenye klabu ya Rotterdam na sasa atarejea mzigoni baada ya kukubali kwenda kuinoa Feyenoord, timu ambayo imetinga hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Straika huyo wa zamani wa Arsenal na Manchester United aliripotiwa kwamba atasaini mkataba hadi 2027 na ataungana na Rene Hake, ambaye hivi karibuni alikuwa kocha msaidizi wa Erik ten Hag alipokuwa Old Trafford. Kwenye kibarua hicho, Van Persie atachukua mikoba ya Pascal Bosschaart, ambaye alikuwa akiinoa timu hiyo kwa muda baada ya Brian Priske kufutwa kazi mapema mwezi huu.
Feyenoord kwa sasa inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Eredivisie, ambapo imejaribu kuzoea maisha mapya bila ya huduma ya kocha wao wa zamani Arne Slot, aliyetimkia Liverpool.
Kwa sasa ikiwa pointi 14 nyuma ya vinara wa ligi hiyo, Ajax, Feyenoord imeonekana kuwa na matumaini makubwa baada ya kutinga hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuinoa AC Milan kwenye mechi ya mchujo.
Alipokuwa kwenye kikosi cha Heerenveen, Van Persie alikuwa na wastani wa ushindi wa asilimia 34 tu baada ya kushinda mechi tisa kati ya 26 na alipoteza 11. Na sasa anarudi kwenye klabu ambayo alianzia maisha yake ya ukocha. Van Persie aliichezea timu hiyo pia mechi 122 katika awamu zake mbili, akifunga mabao 46 kabla ya kustaafu 2019 na kuwa msaidizi wa Dick Advocaat mwaka mmoja baadaye kabla ya kwenda kuchukua majukumu ya kutoa timu ya U-16. Baadaye alipandishwa kuzinoa U18 na U19, lakini aliondoka Mei 2024 kwenda kuchukua kazi ya kuinoa Heerenveen.