Van Dijk kutundika daruga bado sana!
Muktasari:
- Van Dijk ni miongoni mwa mastaa wa Liverpool ambao mikataba yao inamalizika mwisho wa msimu huu pamoja na Mohamed Salah na Trent Alexander-Arnold.
LIVERPOOL, ENGLAND: BEKI wa Liverpool, Virgil van Dijk amedai kuwa ana “miaka mitatu au minne” mbele ya kucheza soka la kiushindani wakati mkataba wake wa sasa ukitarajiwa kumalizika mwisho wa msimu.
Van Dijk ni miongoni mwa mastaa wa Liverpool ambao mikataba yao inamalizika mwisho wa msimu huu pamoja na Mohamed Salah na Trent Alexander-Arnold.
Hata hivyo, kabla ya hapo, mwezi ujao, watatu hao watakuwa na haki ya kufanya mazungumzo na timu za nje ya England.
Wakati sakata la lini mastaa hao tegemeo watasaini mkataba mpya beki huyu raia wa Uholanzi amefunguka kwamba ataendelea kuwepo katika soka la kiushindani kwa miaka hiyo jambo linalotoa ishara kwamba anaweza akasaini mkataba mpya.
Akizungumza na Amazon Prime, alisema: “Ninaipenda klabu, klabu inanipenda. Ninapenda mashabiki, mashabiki wananipenda na huo ni msingi mzuri wa kufanikiwa. Kwa maoni yangu, naweza kucheza angalau kwa miaka mingine mitatu au minne katika soka la kiushindani, tutaona hapo baadaye.”
Mwezi huu mapema, Van Dijk alipewa ofa ya mkataba mpya, lakini inaripotiwa kuwa hakukuwa muafaka uliofikiwa.
Katika mahojiano hayo hayo, Van Dijk mwenye umri wa miaka 33, alionyesha wazi kwamba anatamani kubakia Liverpool kwa kauli yake ya kutaka kucheza soka la kiushindani, pia ilikuwa inafifisha tetesi za kwamba anaweza kutimkia Saudi Arabia.
Mapema katika wiki hii, Jamie Carragher, Jamie Redknapp na Les Ferdinand walijadili suala la mikataba ya mastaa hawa watatu wa Liverpool ambapo Carragher alisema angependelea zaidi kuona Van Dijk anabaki alipoambiwa amchague mchezaji mmoja anayependa kuendelea kumuona kati ya hao watatu.
“Ningesema Van Dijk, na sina shaka kwamba Van Dijk na Salah wataendelea kuwepo,” alisema.