Van Dijk ashambuliwa, mwenyewe asingizia upepo
Muktasari:
- Van Dijk alishindwa kuondoa mpira mrefu ulioingia ndani ya eneo la penalti la timu yake, ikimruhusu Alex Scott kupiga pasi kwa Evanilson ambaye aliwapa Bournemouth bao la kwanza.
LIVERPOOL, ENGLAND: BEKI wa Liverpool, Virgil van Dijk amekosolewa vikali baada ya kufanya makosa yaliyosababisha timu yake kupoteza kwa mabao 3-2 mbele ya Bournemouth, Jumamosi usiku licha ya mwenyewe kujitetea upepo ndiyo sababu.
Van Dijk alishindwa kuondoa mpira mrefu ulioingia ndani ya eneo la penalti la timu yake, ikimruhusu Alex Scott kupiga pasi kwa Evanilson ambaye aliwapa Bournemouth bao la kwanza.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi amekuwa akifanya makosa mengi tangu kuanza msimu huu ambao Liverpool wamekuwa na wakati mgumu chini ya Kocha Erne Slot.
Kipindi cha kwanza, Bournemouth ilipiga mpira mrefu kutoka nyuma, ambao ulionekana kuwa rahisi kwa Van Dijk kuuzuia.
Hata hivyo, alishindwa kuugusa mpira vizuri na kusababisha Scott auchukue na kupiga pasi ya bao kwa Evanilson.
Mashabiki wengi katika mitandao ya kijamii walionyesha kukasirishwa na hali hiyo na mmoja kutoka mtandao wa X zamani Twitter, amesema: Huyu jamaa amechoka, apumzishwe," mwengine akaongeza; "Hii sio sawa Van amefanya nini pale."
Hata hivyo, akizungumzia tukio hilo, kupitia Sky Sports, Van Dijk amesema: “Bao la kwanza, nadhani lilikuwa mpira mgumu kuucheza kutokana na hali iliyokuwepo. Upepo ulikuwa changamoto. Ninakubali kuchukua lawama zote ingawa ulikuwa mpira mgumu kuucheza."
Kipigo hicho kilikuwa ni mwendelezo wa mwenendo mbaya wa Liverpool kwa msimu kwa sasa ikishika nafasi ya nne na tofauti ya pointi 15 dhidi ya vinara Arsenal hali inayozidi kuweka matatani kibarua cha Slot ambaye ametajwa mara kadhaa kuwa huenda akafukuzwa.